Dstv kuisogeza Afcon nyumbani

08Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Dstv kuisogeza Afcon nyumbani

ZIKIWA zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2019) kuanza huko nchini Misri, Kampuni ya MultiChoice Tanzania (DStv)-

Baadhi ya wachezaji wa zamani Timu ya Taifa (Taifa Stars) ambao walishiriki katika Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 1980), wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Dk. Yusuf Singo (wa pili kulia) pamoja na maofisa wa Kampuni ya Multihoice Tanzania katika uzinduzi wa kampeni ya 'DSTV Tupogo' jijini Dar es Salaam jana. PICHA: MPIGAPICHA WETU

imetangaza rasmi kampeni maalumu kwa Watanzania itakayowawezesha kushuhudia michezo yote 52 ya michuano hiyo kupitia chaneli za Supersport zilizo katika mfumo wa HD.

Akizungumza katika hafla ya kuzindua kampeni hiyo ya DStv ijulikanayo kama ‘DStv Tupogo’, Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania, Jacqueline Woiso, alisema kuwa kampuni yao inafuraha kuwapatia burudani hiyo mashabiki wa soka wa hapa nchini ambao wataiona timu yao ya Taifa (Taifa Stars) ambayo itashiriki fainali hizo.

"Tuna furaha kubwa kwa nchi yetu kupata fursa ya kushiriki katika michuano hii ya kimataifa baada ya takribani miaka 39 tangu iliposhiriki kwa mara ya mwisho mwaka 1980. Na kama ilivyo ada, ni jukumu letu na la kila Mtanzania kuhakikisha kuwa tunawatia moyo vijana wetu na kuifanya nchi yetu ifanye vizuri katika michuano hii ya kimataifa.

Kwa kuzingatia hilo, DStv imehakikisha kuwa mechi zote za michuano hii ya kimataifa zitarushwa mubashara DStv kupitia chaneli za Supersport na kwa lugha adhimu ya Kiswahili, Dstv imehakikisha kuwa mechi hizo zinaonekana katika vifurushi vyote kuanzia kile cha chini kiitwacho DStv Bomba ambacho gharama yake ni Sh. 19,000 tu. “Tumehakikisha kuwa mechi hizi zinakuwepo hadi kwenye kifurushi cha chini kabisa ili kuwawezesha watanzania wengi kushuhudia mtanange huo na kuwa sehemu ya historia ya nchi yetu kwani tunashiriki baada ya zaidi ya miaka 30”, alisema Woiso.

Alisema kuwa mechi hizo zitatangazwa kwa lugha ya kiswahili kwa kutumia watangazaji maarufu wa hapa nchini huku pia wakimtambulisha mchamuzi mpya mwanamke ambaye ni Salama Jabir atakayeungana na wakongwe, Aboubakar Liongo, Ibrahim Maestro, Edo Kumwembe, Maulid Kitenge  na Oscar Oscar.

Naye Mkuu wa Masoko wa MultiChoice Tanzania, Ronald Shelukindo alisema, “Wateja wa DStv pia wataweza kupokea matangazo ya moja kwa moja kwa kupitia application ya “DStv Now” kupitia katika vifaa mbalimbali ikiwamo  simu ya mkononi, lap top au tablet na televisheni ya kawaida”.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Dk. Yusuph Singo alisema kuwa kitendo cha DStv kuonyesha mubashara michuano hiyo ni cha kupongezwa kwani ni sifa kubwa kwa nchi yetu. Singo alisema kuwa mchango mkubwa unaotolewa na MultiChoice Tanzania katika sekta ya michezo umechangia sana katika kukuza michezo na kuliletea taifa sifa kubwa.

Habari Kubwa