Dynamos waikacha Simba, sasa watacheza na Mtibwa

10Dec 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Dynamos waikacha Simba, sasa watacheza na Mtibwa

TIMU ya Power Dynamos ya Zambia imeahirisha safari ya kuja Tanzania kumenyana na Simba katika mchezo wa kirafiki uliopangwa kufanyika Jumatatu uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

TIMU ya Power Dynamos ya Zambia.

Kwa sababu hiyo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Hajji Sunday Manara aliiambia Nipashe jana kwamba Wekundu wa Msimbazi watamenyana na Mtibwa Sugar badala ya Power Dynamos.

Mchezo huo utakaochezwa siku ya sherehe za Maulid kuazimisha kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W.) ni maalumu kwa kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog kumjaribu kipa mpya, Daniel Agyei kutoka Medeama SC ya Ghana.

Manara alisema kwamba kikosi cha Simba kinaendelea vizuri na mazoezi katika kambi yake ya Morogoro chini ya Kocha Mkuu, Mcameroon, Joseph Marius Omog anayesaidiwa na Mganda, Jackson Mayanja.

Manara amesema kwamba kikosi kitawasili Dar es Salaam asubuhi ya kuamkia mchezo huo, Jumatatu – na baada ya hapo kitaendelea na maandalizi ya mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mzunguko wa pili dhidi ya Ndanda FC mjini Mtwara.

Wachezaji wa Simba walioko kambini Morogoro ni makipa; Vincent Angban, Peter Manyika, Daniel Agyei, na Dennis Richard, mabeki; Hamad Juma, Janvier Bokungu, Abdi Banda, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Emmanuel Semwanza, Malika Ndeule, Novaty Lufunga na Method Mwanjali.

Viungo ni Awadh Juma, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Said Ndemla, Mussa Ndusha, Muzamil Yassin, Jamal Mnyate, Shizza Kichuya na washambuliaji Frederick Blagnon, Laudit Mavugo, Ame Ally na Ibrahim Hajib na Hajji Ugando.

Mchezaji pekee anayekosekana Simba kwa sasa ni beki Mganda, Juuko Murshid, ambaye ana ruhusa maalum, yupo na timu yake ya taifa inayojiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Gabon mwezi ujao.

Simba ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara katika nafasi ya kwanza kwa pointi zake 35, mbili zaidi ya mabingwa watetezi, Yanga.

Habari Kubwa