Akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua tamthilia hiyo, Mkuu wa Vipindi wa EATV, Lydia Igarabuza alisema kituo chake kimeongeza vipindi kwa watazamaji wake na wanaamini tamthilia hiyo itawaelimisha na kuwafurahisha.
"Pia hii ni sehemu ya kuonyesha vipaji vya Watanzania kwa nchi za Afrika Mashariki ambako kote huko kituo cha EATV matangazo yake yanaonekana," alisema Igarabuza.
Alisema kuwa tamthilia hiyo itaonyeshwa kwa nusu saa kwa siku nne mfululizo kuanzia Jumatatu hadi Alhamisi (kuanzia saa 12:30 jioni mpaka saa 1:00).
Mmoja wa wahusika kwenye tamthilia hiyo iliyotengenezwa na Jason Production ya Dar es Salaam, Mrisho Salehe maarufu kwa majina ya Tito na Carlos, alisema kuwa tamthilia hiyo itaonyesha vitu vinavyotokea kwenye familia.
"Hii ni tamthilia itakayomgusa mtu yeyote kwa sababu yatakayoonekana ni yale ambayo yako kwenye familiza zetu, ndiyo maana tukaiita 'Siri za familia'," alisema Carlos.