Evra afunguka mwalimu kumnyanyasa kingono

25Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Evra afunguka mwalimu kumnyanyasa kingono

MLINZI wa zamani wa Manchester United, Patrice Evra, amesema alinyanyaswa kingono na mwalimu wake alipokuwa katika umri wa kupevuka (balehe).

Evra, mwenye umri wa miaka 40, alizungumzia hilo wazi katika mahojiano na gazeti la The Times la Uingereza kabla ya kutoa kitabu chake, juzi.

Alielezea ni kwa nini hakuwahi kuzungumzia suala hilo hadi sasa.

"Kwanza nilipoandika kitabu, sikuelezea hadithi yote kwa sababu nilikuwa nina aibu na kuogopa ni nini watu wangefikiria," alisema Evra.

"Sasa ninataka kusema kwa sababu sitaki watoto wawe katika hali yangu na kuhisi kuaibika, wakifikiria kwamba hawana ujasiri, ni suala la utayari wa akili wa kuzungumzia suala hili.

"Kwa hiyo ninataka kuwafanya watoto wawe na ujasiri na wasijilaumu wenyewe, kwa sababu kila mara nimekuwa nikijilaumu mwenyewe.

"Sina aibu ya kusema kuwa nilihisi kama muoga kwa miaka mingi kwa sababu sikuwahi kuzungumzia unyanyasaji huu wazi. Kilikuwa ni kitu kizito kifuani mwangu. Lakini sikukifanya mwenyewe. Ninafanya kwa ajili ya watoto wengine."

Evra, ambaye alikulia katika kitongoji cha Les Ulis karibu na Jiji la Paris nchini Ufaransa, amesema unyanyasaji huo dhidi yake ulifanyika katika nyumba ya mwalimu, ambako aliiishi ili kupunguza muda wa usafiri baina ya nyumbani kwao na shuleni.

Alimwambia tu mama yake wiki mbili zilizopita, na akasema alikataa ombi la mama yake ambaye alimtaka asijadili jambo hilo katika kitabu.

"Ni sasa wakati nina umri wa miaka 40 ndio nimemwambia mama yangu," alisema. "Ulikuwa ni mshtuko mkubwa kwake. Alikasirika sana. Aliniambia pole. Alisema, 'Usiweke hili katika kitabu chako, ni jambo la kibinafsi'.

Habari Kubwa