Eymael awatia mzuka Yanga

10Jul 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Eymael awatia mzuka Yanga

KOCHA Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, amesema anajua kikosi chake hakina namna yoyote ya kuweza kushiriki michuano ya Kimataifa endapo hawatatwaa ubingwa wa FA, na sasa ameweka bayana kwamba lazima washinde mchezo wao dhidi ya Simba.

KOCHA WA YANGA ,LUC EYMAEL AKIWA NA WACHEZAJI WA TIMU HIYO:PICHA NA MTANDAO

Yanga wanakutana na Simba Jumapili kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Nipashe, Eymael alisema matokeo ya mechi yao ya juzi dhidi ya Kagera Sugar ya bao 1-0 yalikuwa ni maandalizi kwa ajili ya mchezo wao huo dhidi ya Simba na ni lazima washinde.

Alisema anaamini mchezo huo utakuwa mgumu kwa dakika zote 90, lakini amewaandaa wachezaji wake kumaliza kazi mapema.

"Hii mechi itakuwa ngumu sana, kwa sababu Simba wanataka kulipa kisasi kwani tuliwafunga mchezo uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini wote tunataka kuingia fainali na kutwaa ubingwa huu,” alisema.

"Sisi mchezo huu una umuhimu mkubwa sana kwetu, kwani inaweza ikawa njia ya kushiriki michuano ya kimataifa, na tumejiandaa tunamaliza kazi mapema," alijigamba Eymael.

Alisema kuna mambo mengine hawezi kuweka wazi kikubwa wanaendelea na maandalizi kuhakikisha kikosi chake kinakuwa kwenye hali nzuri.

Kocha huyo raia wa Ubelgiji aliongeza kusema, hawataki kupoteza mchezo huo sababu ndio nafasi pekee ya wao kuweza kufuzu kushiriki michuano ya kimataifa msimu huu.

Akizungumzia wachezaji wake, alisema kiungo wake, Haruna Niyonzima anaendelea vizuri, lakini ni mapema kuweka wazi kuwa atacheza kwenye mchezo huo, kwa sababu anaangalia kwanza ufiti wake baada ya kuumia katika mchezo na Biashara.

Katika mchezo huo, Yanga watakuwa na kazi moja tu ya kuhakikisha wanashinda ili kupata nafasi hiyo ya kushiriki michuano ya kimataifa.

Yanga watamtegemea zaidi kiungo wao, Bernard Morrison, ambaye ndiye aliyewalaza na viatu wekundu hao wa Msimbazi Machi 8 mwaka huu, akifunga bao pekee kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara mzunguko wa pili.

Timu hizo zilipokutana Machi 8 mwaka huu, ilikuwa mechi ya kwanza kwa kila kocha kukaa kwenye benchi kushuhudia timu hizo zikikwaana.

Huo utakuwa mchezo wa tatu katika msimu huu, kwani mchezo wa kwanza ulikuwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mzunguko wa kwanza, ambapo timu hizo zilitoka sare ya kufungana mabao 2-2, kabla ya Morrison kuwaadabisha Simba kwa bao 1-0 katika mchezo wa pili.

Habari Kubwa