Eymael kurejea kibaruani Yanga

22May 2020
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
Eymael kurejea kibaruani Yanga

KOCHA Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, anatarajiwa kurejea nchini wakati wowote kuanzia leo ili kuungana na kikosi chake baada ya kukamilika kwa maandalizi ya usafiri wa ndege.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Luc Eymael:PICHA NA MTANDAO

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya mtandao Luck alisema ameshafanya mawasiliano na uongozi ili kujua utaratibu mzima wa tiketi pamoja na ndege itakayomfaa kwa safari.

"Nimeshukuru kusikia ndege zimeanza kuruhusiwa kuja Tanzania, binafsi nimefarijika mipango ya safari ikikamilika nitarudi kuendelea na ligi," alisema Eymael.

Aliongeza kwa muda wote alipokuwa Afrika Kusini alikuwa akiwasiliana mara kwa mara na wachezaji wake kufahamu utekelezaji wa programu za mazoezi na hana wasiwasi na uwezo wao wa kurejea kumalizia msimu.

"Lengo ni kuipa mafanikio klabu yetu kwa kushika nafasi ya juu katika msimamo wa Ligi Kuu, tuombe taratibu zikamilike kila kitu kitakuwa sawa, " Eymael aliongeza.

Naye nahodha msaidizi wa Yanga, Juma Abdul, alisema anatamani kurudi uwanjani mapema ili kuendelea na majukumu yake.

Beki huyo alisema amekuwa na 'kiu' na mashabiki wake baada ya kukaa kwa muda mrefu bila kucheza, kutokana na ligi hiyo kusimamishwa ili kupisha maambukizo ya corona (COVID 19).

Habari Kubwa