Fainali UEFA Liverpool vs Madrid Darajani Dar

18May 2022
Nipashe
Fainali UEFA Liverpool vs Madrid Darajani Dar
  • ***Serikali yasema itaonyeshwa mubashara Daraja la Tanzanite pamoja na Filamu ya Royal Tour huku...

KUELEKEA mechi ya Fainali ya 67 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (Uefa Champions League Fainal 2022) itakayopigwa Uwanja wa Stade de France nchini Ufaransa Mei 28, mwaka huu,...

... Watanzania watapata fursa ya kushuhudiwa mtanange huo mubashara tena bure katika daraja la jipya la Tanzanite jijini Dar es Salaam sambamba na Filamu ya Royal Tour, imeelezwa.

Serikali ndiyo iliyotoa kauli hiyo kupitia kwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa, ambaye amesema mechi hiyo ya fainali itaonyeshwa mubashara nchini kwenye Daraja la Tanzanite kupitia DStv ambapo vivutio mbalimbali vya utalii pia vitaonyeshwa moja kwa moja, hivyo kutoa fursa kwa mamilioni ya wapenzi wa soka kutoka nchi zote za Afrika na dunia kushuhudia mechi hiyo na vivutio vya utalii kutoka Tanzania.

Akizungumza kupitia kipindi cha Powerbreakfast kinachorushwa na Kituo cha Redio cha Clouds Fm, Dar es Salaam jana, Mchengerwa alisema mbali na kurusha mubashara mechi hiyo yenye mvuto mkubwa hapa nchini na duniani kote pia Filamu ya Royal Tour itaonyeshwa kabla ya kuanza mchezo huo ambapo ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kushuhudia tukio hilo la kihistoria.

Mchengerwa alifafanua kuwa wakati wa filamu hiyo ya kihistoria iliyomshirikisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambayo imefungua Tanzania duniani, kutachezeshwa droo ambapo washindi watatu watakaopatikana watatembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini kwa ufadhili wa Bodi ya Utalii nchini (TTB) na Kampuni ya Heinken.

Aidha, amesema dhamira ya serikali kwa sasa ni kuendelea  kutumia sekta za michezo na sanaa kuitangaza Tanzania na vivutio vyake duniani kwa kuwa zimebeba idadi kubwa ya rasilimali za Tanzania na kuongeza kuwa sekta hizo ndiyo nguvu shawishi ya serikali zinazowapa Watanzania wengi zaidi furaha na faraja.

“Nipende kumpongeza rais wetu kwa kazi kubwa sana na mikakati thabiti anayoifanya hivi sasa ya kuifungua Tanzania kupitia sanaa na michezo ambapo hivi karibuni ameandika historia kwa kushiriki moja kwa moja katika kuandaa Filamu ya Royal Tour,” alisema Mchengerwa.

Alitaja baadhi ya mikakati mingine inayofanywa na Rais Samia kuwa ni kuifungua na kuitangaza Tanzania duniani kupitia sanaa na michezo kuwa  ni pamoja na kuandaa mashindano makubwa barani Afrika ya tuzo za wasanii ili  yafanyike hapa nchini  yanayojulikana kama MTV Afrika Awards hapo mwakani,  kuandaa mkutano wa marais wa mashirikisho ya soka utakaohudhuriwa na zaidi ya nchi 54 za Afrika jijini Arusha ambapo Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino, anatarajiwa kuhudhuria pamoja na kufikiria kuandaa mashindano makubwa ya soka Afrika kuanza kufanyika hapa nchini.

Pia, ameongeza kuwa tayari serikali kupitia wizara anayoiongoza inakamilisha michoro kwa ajili ya kujenga kumbi za kisasa za michezo na  maonyesho ya sanaa ambapo moja inatarajiwa kuchukua takriban watu 20,000 jijini Dar es Salaam na nyingine yenye uwezo wa kuchukua watu 15,000 jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Heinken nchini ambayo ndiyo mdhamini mkuu wa tukio hilo, Fatma Mnaro, amefafanua kuwa lengo la kuonyesha mubashara kilele cha UEFA 2022 hapa nchini kupitia DSTv ni kutaka kuwafanya  wapenzi wa soka walione shindano hilo kwa ubora wa hali ya juu kama ambavyo watakavyoshuhudia wale ambao watahudhuria mtanange huo jijini Paris, Ufaransa.

Mnaro aliongeza kuwa pamoja na kurushwa mubashara kwenye Daraja la Tanzanite, kuna sehemu mbalimbali za majiji makubwa ambazo pia zitaonyesha ikiwa ni pamoja na The Cask jijini Mwanza, City Pub jijini Mbeya, Arusha na Capetown Fish Market, Samakisamaki na Triple 777 jijini Dar es Salaam.

 

 

%%%%%%%%

 

 

Habari Kubwa