Farid asubiri leseni kukipiga Hispania

05Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Farid asubiri leseni kukipiga Hispania

BAADA ya kutua klabu yake mpya ya Deportivo Tenerife ya Hispania, nyota wa Tanzania, Farid Mussa, amesema kwa sasa anasubiri kupewa leseni ya kucheza soka katika nchi hiyo ili aanze kuitumikia timu yake.

Farid anasubiri leseni hiyo kutoka kwa Shirikisho la Soka Hispania (RFEF).

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya mtandao, Farid, alisema tangu afike Hispania amekuwa akifanya mazoezi pamoja na wachezaji wenzake kwenye timu hiyo.

"Nashukuru ndugu yangu naendelea vizuri, nimeanza mazoezi na wenzangu, lakini kwa sasa sijaanza kucheza mechi nasubiri kukamilisha taratibu za huku ili nianze kucheza, nasubiri kupewa leseni na Chama [Shirikisho la] Soka hapa Hispania," alisema Farid.

Alisema anategemea kupata leseni hiyo wakati wowote kuanzia sasa.

Farid amejiunga na timu hiyo kwa mkopo wa muda mrefu akitokea kwa mabingwa wa soka Afrika Mashariki, Azam FC.

Nyota huyo kwa mara ya kwanza alienda kwenye klabu hiyo Aprili mwaka jana kwa ajili ya kufanya majaribio ambapo alifanikiwa kuwashawishi makocha wa klabu hiyo waliomtaka kwenda kuichezea timu hiyo.

Habari Kubwa