Farid sasa aipeleka Azam Hispania

20Nov 2016
Mahmoud Zubeiry
Nipashe Jumapili
Farid sasa aipeleka Azam Hispania

MTENDAJI Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba sasa atasafiri hadi Hispania kwenda kuzungumza na klabu ya Deportivo Tenerife juu ya suala la mchezaji wao, Farid Malik.

Kiungo chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Farid amekwama kwenda kujiunga na Deportivo Tenerife, licha ya kupata kibali rasmi cha kufanya kazi nchini Hispania.

Akizungumza na Nipashe jana mjini Dar es Salaam, Farid alisema baada ya kukwama kabisa kupatiwa visa ubalozi wa Hispania hapa nchini, sasa ameambiwa uongozi wa Azam utakwenda kuonana na uongozi wa Deportivo Tenerife.

“Bado sijafanikiwa kupata visa, wameniambia Saad (Kawemba) anakwenda Hispania kukutana na viongozi wa Deportivo Tenerife.
Sasa inabidi nisubiri aende akazungumze nao, kisha atanifahamisha. Kwa sasa niko njia panda,”alisema jana Farid.

Haijulikani ni nini haswa kinamkwamisha Farid kupata visa, kwani mwezi uliopita Azam FC ilitoa taarifa ya kupata kibali cha mchezaji huyo kufanya kazi Hispania, maana yake alikuwa huru kwenda kuanza kujiunga na timu hiyo ya Daraja la Kwanza.

Azam FC imemtoa kwa mkopo Farid kwenda CD Tenerife kwa makubaliano maalum. Hilo lilikuja baada ya Farid kufuzu majaribio katika klabu hiyo katikati ya mwaka alipokwenda na mkurugenzi wa klabu yake, Yussuf Bakhresa.

Farid alitua Hispania Aprili 21 baada ya kuichezea Azam FC katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Esperance mjini Tunis, Tunisia ikifungwa 3-0 na kutolewa kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya awali kushinda 2-1 Dar es Salaam.

Ilimchukuwa wiki moja tu Farid kuwakuna kwa kipaji chake makocha wa Tenerife na kutaka kumnunua, lakini Azam ikataa na kuamua kumtoa kwa mkopo.

Azam FC haijamsajili Farid katika kikosi chake cha Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kwa kuwa imemtoa kwa mkopo Tenerife ambayo tayari imemuombea hadi Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).

Kutokana na kutocheza tangu Agosti, Farid ametemwa hadi timu ya Taifa, Taifa Stars na wasiwasi ni kwamba kutaathiri zaidi kiwango cha kijana huyo aliyekuwa anainukia vizuri katika soka la kimataifa.

Habari Kubwa