Fedha za Okwi ni 'jipu' lisilotumbuka

11Feb 2016
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Fedha za Okwi ni 'jipu' lisilotumbuka

BADO hadithi ni ile ile, uongozi wa Simba umeendelea kusubiri malipo ya aliyekuwa mshambuliaji wake Mganda, Emmanuel Okwi kutoka kwa klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia.

Emmanuel Okwi (kushoto) akiwa uwanjani

Simba ilimuuza Okwi kwa dau la Dola za Marekani 300,000 (zaidi ya Sh. milioni 600) tangu mwaka juzi na hadi kufikia jana haijapokea kiasi chochote cha malipo hayo huku mchezaji huyo akiwa tayari ameshaihama timu hiyo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara alisema kuwa bado klabu yao haijapokea taarifa nyingine kutoka Etoile du Sahel kuhusiana na fedha hizo licha ya muda waliopewa na Fifa kumalizika.

Manara alisema kuwa Simba haitachoka kuulizia fedha hizo na imepanga kuandika barua nyingine na kuipeleka katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili wawasiliane na Fifa kuwakumbusha madai yao.

"Inasikitisha kwa kweli, hakuna barua wala maelezo mapya tuliyopokea kutoka kwa Etoile du Sahel, ila kwa sababu ni haki yetu, tutaandika barua nyingine kabla ya wiki haijamalizika," alisema Manara.

Aliongeza kuwa bado msimamo wa Simba uko pale pale wa kutaka kulipwa fedha hizo kwa awamu moja na hiyo imetokana na usumbufu walioupata kwa klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Tunisia.

"Hawa ndiyo wametufanya pia tuwaandikie barua mapema TP Mazembe kuwakumbusha mgawo wetu baada ya kumuuza Samatta (Mbwana) Ubelgiji," aliongeza kiongozi huyo.

Kwa mujibu wa barua ya Fifa kwa Shirikisho la Soka Tunisia (FTF) na nakala yake kwenda TFF, klabu ya Etoile du Sahel inashitakiwa kwa kuvunja kanuni kwa mujibu wa ibara ya 64 ya kanuni za nidhamu za Fifa (Fifa Disciplinary Code).

Etoile Sportive du Sahel wametakiwa kulipa mara moja kiasi cha Dola za Marekani 300,000 na riba ya asilimia 2% kwa kila mwaka kama ilivyoelekezwa na uamuzi ya Jaji mmoja wa Kamati ya Nidhamu za Wachezaji uliotolewa Novemba 20, 2014.

Tangu wakati huo TFF imekua ikiwasiliana na FTF na FIFA kwa niaba ya klabu ya Simba ambao ni mwanachama wake. Ikiwa klabu hiyo ya Tunisia haitailipa Simba fedha hizo, itakuwa kwenye hatari ya kushushwa daraja au kupokwa alama kwenye ligi.

Habari Kubwa