Fei Toto akili zote sasa kwa Lesotho

22Oct 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Fei Toto akili zote sasa kwa Lesotho

NYOTA wa Yanga, Feisal Salum 'Fei Toto', amesema tayari anauwaza mchezo wa kufuzu fainali za Afrika dhidi ya Lesotho utakaochezwa mwezi ujao.

NYOTA wa Yanga, Feisal Salum 'Fei Toto' picha na mtandao

Kiungo huyo ameliambia Nipashe jana kuwa kiu ya kutaka kucheza fainali hizo za Afrika zinamfanya kuuwaza mchezo huo muhimu.

Alisema mchezo huo ni muhimu sana kwa Tanzania kwa kuwa ushindi huo pekee utawasogeza karibu kabisa na kufuzu kwa fainali hizo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1980.

"Wachezaji wote wa Tanzania bila kujali kama tutakuwapo, tunatamani kuona tunafuzu fainali zijazo za Afrika, mchezo na Lesotho ndio tunaoufikiria zaidi," alisema Fei Toto.

Fei Toto aliingia kipindi cha pili kwenye mchezo dhidi ya Cape Verde na kuonyesha kiwango cha juu kilichomgusa kocha wa timu hiyo, Emmanuel Amunike.

Kwa sasa Stars inajiandaa na mchezo dhidi ya Lesotho utakochezwa ugenini Novemba 16, mwaka huu.

Ushindi utaifanya Stars kufikisha pointi nane na kama Cape Verde itapoteza dhidi ya Uganda mechi ijayo, basi Tanzania itakuwa imefuzu fainali hizo zitakazofanyika Cameroon hapo mwakani.

Katika Kundi hilo la L, Uganda ipo kileleni ikiwa na pointi 10, ikifuatiwa na Stars yenye tano huku Cape Verde ikiwa nafasi ya tatu na pointi zao nne wakati Lesotho ikiburuza mkia na pointi mbili. 


Habari Kubwa