Fernandes achambua Ronaldo kurudi United

09Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Fernandes achambua Ronaldo kurudi United
  • ***Tunajua ari itakuwa juu, tunajua nini anachoweza kutupa sisi, kila mmoja anajua Cristiano ana...

KURUDI kwa Cristiano Ronaldo pale Old Trafford kutaongeza ujasiri na kuisaidia Manchester United kushinda mataji, kwa mujibu wa Bruno Fernandes.

Fernandes alikuwa mchezaji nguzo wa United msimu uliopita, akifunga mabao 18 na kutoa pasi za mwisho 12 kwenye Ligi Kuu England wakati kikosi hicho cha kocha, Ole Gunnar Solskjaer kikimaliza nafasi ya pili kwenye msimamo.

Ronaldo sasa ameungana na mchezaji mwenzake huyo wa timu ya Taifa ya Ureno, aliyerudi hapo Manchester baada ya miaka 12, awali akifunga mabao 118 kwenye mechi 292 kwenye mashindano yote katika kipindi chake cha kwanza kucheza hapo.

Na Fernandes, ambaye alionyesha kiwango cha juu na kutengeneza pasi tano muhimu na asisti moja wakati Ronaldo akikosekana kwenye mchezo wa timu ya Taifa ya Ureno dhidi ya Azerbaijan, amesifia ubora na ujasiri wa mfungaji huyo wa wakati wote wa timu ya taifa.

"Tunajua kwamba, ari itakuwa juu, kila mmoja anajua Cristiano ana furaha kubwa na kujiamini sana bada ya kurudi tena hapa," alisema Fernandes akiiambia RTP3.

"(Sisi) wachezaji ni sehemu ya ujasiri huo, tunajua nini anachoweza kutupa sisi. Malengo yetu ni makubwa na Cristiano pia, kwa sababu nilichoongea naye ni kuhusu kushinda mataji.

"Malengo yetu yatabaki kuwa hivyo, kwa uwapo wa Cristiano, kuna kitu cha ziada cha kutusaidia kufika kule tunakotaka kwenda."

Ronaldo mwenye miaka 36, anaweza kucheza mchezo wake wa kwanza Septemba 11, mwaka huu dhidi ya Newcastle United, klabu ambayo ndio pekee kwenye Ligi Kuu England aliyoifunga mabao matatu ‘hat-trick’ kabla ya kuondoka Manchester mwaka 2009.