Fifa yaikamata pabaya Simba, yaitaka kulipa Sh. mil. 70

07May 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Fifa yaikamata pabaya Simba, yaitaka kulipa Sh. mil. 70

KLABU ya Simba imepigwa faini Sh. milioni 4.5 na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kupuuza maagizo ya Idara ya Utatuzi wa Migogoro la kumlipa beki wake wa zamani, Donald Musoti wa Kenya.

Rais wa Simba Evans Aveva na msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara.

Kamati ya idara hiyo iliyokutana na Aprili 20 mwaka huu Zurich, Uswisi pia ilitumia Sh. milioni 1.5 kwa ajili ya gharama za kikao cha kufuatilia utekelezaji sakata la mchezaji huyo. Simba imeelezwa kupuuza kumlipa Musoti kwa wakati tangu mkataba wake ulipovunjwa.

Musoti alisajiliwa na Simba msimu wa 2014/15 na kuachwa na aliishitaki klabu hiyo na Fifa akitaka kulipwa Sh. milioni 62.8 na kiasi kingine Sh. milioni 1.2 zilizobaki katika usajili.

Felix Majani, Mwanasheria wa Musoti, ambaye pia ni mmoja wa wanasheria wa Fifa alifungua kesi katika shirikisho hilo kuwashtaki Simba kwa kukiuka makubaliano ya mkataba na mteja wake.

Majumuisho ya fedha zote, yaani faini, gharama za kikao cha kuamua sakata hilo, fedha ya usajili iliyobaki na fidia na ni zaidi ya Sh. milioni 70, ambazo klabu hiyo ya inatakiwa kulipa ndani ya siku 30 kuanzia tarehe ya kupokea barua hiyo jana Mei 6, vinginevyo itashushwa daraja.

Rais wa Simba, Evans Aveva alisema jana wameshangazwa kuona deni hilo limeongezeka wakati tayari walishaanza mawasiliano na mwanasheria wa Musoti.Aidha, alisema deni wanalofahamu ni dola 15,000, lakini wameshangaa kuongezeka hadi milioni 62.

Habari Kubwa