Fifa yamfungia Rais CAF miaka mitano

24Nov 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Fifa yamfungia Rais CAF miaka mitano
  • ***Sababu zabainishwa, baadhi ya viongozi wa mashirikisho ya soka Afrika watajwa kuhongwa, pia apigwa faini ya Sh. milioni 507 huku...

RAIS wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), Ahmad Ahmad, amefungiwa kujihusisha na masuala yoyote ya soka kwa kipindi cha miaka mitano na FIFA kutokana na matumizi mabaya ya fedha.

Kifungo hicho kilitangazwa wakati ofisa huyo wa Madagasca akiwa kwenye kampeni zake za kutaka kuchaguliwa tena kwa miaka minne zaidi kushika nafasi hiyo CAF, inayompa pia fursa ya kuwa Makamu wa Rais wa FIFA.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kamati ya Maadili ya FIFA, iligundua "Ahmad alikuwa amekiuka wajibu wake wa uaminifu, kwa kutoa zawadi na mafao mengine, kushindwa kusimamia fedha na alitumia vibaya nafasi yake kama Rais wa CAF."

Ahmad, ambaye ni ofisa wa zamani wa serikali ya Madagascar, pia kifungo hicho cha FIFA kwake, kimekwenda sambamba na faini ya dola za Marekani 220,000 sawa na Sh. milioni 507.9 za Tanzania.

Muhula wa kwanza wa miaka minne wa Ahmad ulikuwa umegubikwa na tuhuma nyingi za matumizi mabaya ya fedha na utovu wa nidhamu katika Makao Makuu ya Shirikisho la Soka la Afrika huko Cairo, Misri.

"Uchunguzi juu ya mwenendo wa Ahmad katika nafasi yake kama Rais wa CAF katika kipindi cha kuanzia mwaka 2017 hadi 2019, ulihusu masuala yaliyohusiana na utawala, pamoja na kuandaa na kufadhili hija ya kwenda Makka, kuhusika kwake katika shughuli za CAF na kampuni ya vifaa vya michezo na shughuli zingine,” FIFA ilieleza katika taarifa yake.

CAF ilionekana kulipa karibu dola za Marekani 100,000 sawa na Sh. milioni 230.8 za Tanzania, kwa watu 18, pamoja na Ahmad na wakuu wa baadhi ya mashirikisho 54 ya kitaifa ya soka barani Afrika, kusafiri kwa hija huko Saudi Arabia.

Ili Ahmad aweze kugombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi ujao wa CAF utakaofanyika Machi 12, mwakani jijini Rabat, Morocco, ana nafasi ya kukata rufani katika Mahakama ya Usuluhishi ya Mambo ya Michezo (CAS), pindi tu atakapopokea uamuzi mzima uliofikiwa, mchakato ambao utachukua siku 60.

Habari Kubwa