Gadiel aendelea kuivuruga Yanga

06Jul 2019
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
Gadiel aendelea kuivuruga Yanga

IKIWA leo ndio siku ya mwisho ambayo beki, Gadiel Michael, amewapa viongozi wa Yanga kukamilisha mahitaji yake anayoyataka, uongozi wa klabu hiyo umemtaka mchezaji huyo achague timu anayoitaka kuitumikia katika msimu ujao.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Dismas Ten.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Dismas Ten, alisema bado wanaendelea kuzungumza na Gadiel ili aweze kusaini mkataba mpya, lakini ameweka wazi kwamba beki huyo yupo kuchagua klabu anayotaka kuitumikia.

“Gadiel yupo huru, kwa sababu mkataba wake umeisha tangu mwezi uliopita, sisi kama Yanga tulimpa nafasi ya kuchagua timu anayoitaka, kwa hiyo ni ngumu kuzungumzia suala lake kwa sasa,”alisema Dismas.

Kiongozi huyo aliwataka mashabiki wa Yanga kutokuwa na wasiwasi kwa sababu klabu yao imeshasajili wachezaji wazuri ambao wataongeza ushindani ndani ya klabu hiyo katika msimu ujao.

Alisema kuwa kikosi chao kinatarajia kuanza mazoezi kesho baada ya wachezaji wao waliokuwa likizo na wale wapya kutarajia kuripoti jijini.

“Leo (jana) tunatarajia kuanza kupokea wachezaji wetu ambao wanatoka mikoani na wale wa kimataifa kwa ajili ya kujiandaa kuanza rasmi mazoezi Jumapili, ila tunatarajia kutangaza programu zetu zitakavyokuwa kuanzia Jumatatu baada ya taratibu kukamilika,” aliongeza kiongozi huyo.

Hata hivyo, taarifa za ndani zilizopatikana jijini zinaeleza kwamba beki huyo wa zamani wa Azam FC, tayari ameshasaini mkataba wa kuitumikia Simba na kinachosubiriwa ni muda rasmi wa kutangazwa.

"Muda tu ndio utaongea, kiukweli tayari Gadiel alishasaini Simba, ila huu utaratibu wao mwaka huu, umejua kuwaweka wanachama roho juu," alisema mmoja wa viongozi wa juu wa Yanga.

Alisema nyota huyo amekuwa akiwazungumzia viongozi wake kama ambavyo aliyekuwa mshambuliaji wao, Ibrahim Ajibu, alivyokuwa anafanya.

Habari Kubwa