Gharama kuishuhudia Stars Afcon hizi hapa

11Jun 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Gharama kuishuhudia Stars Afcon hizi hapa

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, ameendelea kuwahamasisha wabunge kwenda Misri kushuhudia fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019, huku akiweka wazi gharama zake kuwa ni Dola za Marekani 1490 (sawa na Sh. milioni 3.4) kwa kila mmoja kwa siku 10.

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai.

Fainali hizo zinatarajiwa kuanza Juni 21, huku timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' iliyopangwa Kundi C ikianza kusaka nafasi ya kutinga robo fainali kwa kucheza dhidi ya Senegal Juni 23, na kisha kuivaa Kenya siku nne baadaye kabla ya Julai Mosi, mwaka huu kumaliza mechi za hatua ya makundi kwa kuvaana na Algeria.

Akitoa matangazo bungeni jijini Dodoma jana, Spika Ndugai alisema gharama za safari zinategemea na chaguo la mbunge kama anataka kwenda awamu zote mbili au moja.

“Awamu ya kwanza ambayo ni siku nne ni Dola za Marekani 720, hii ni pamoja na usafiri na mambo mengine hadi kupelekwa uwanjani kutoka hotelini.

"Awamu ya pili ni siku sita ambayo ni Dola za Marekani 770, hivyo ukitaka kwenda zote mbili ni zaidi ya Dola za Marekani 1400," Spika Ndugai alisema.

Aliongeza kuwa wabunge wanaweza kushiriki awamu moja wapo na kuwataka kujiandikisha na kulipia mapema.

“Tujiandikishe mapema ili tuweze kwenda kushuhudia timu yetu kwenye fainali hizi, hawa wa awamu ya kwanza wa siku nne na mimi nitalipia nitaenda.

"Tunaweza kuwa pamoja, naomba tuunge mkono timu yetu, ni miaka mingi sana hatujafika Afcon," Ndugai alisisitiza.

Alibainisha kuwa wachezaji wakicheza huku wakiona wabunge wao huko Misri wakiwaunga mkono, watapata nguvu zaidi.

Tanzania ilifuzu kwa mara ya kwanza kushiriki mashindano hayo makubwa mwaka 1980 na baada hapo haikufanikiwa tena kushiriki.

Habari Kubwa