Gomes ahamishia hesabu Ligi Kuu

10Apr 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Gomes ahamishia hesabu Ligi Kuu

BAADA ya kukamilisha mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes, amesema sasa hesabu zake anazihamishia kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kikosi cha Simba ambacho jana usiku kilikuwa kinavaana na vigogo wa Misri, Al Ahly mara baada ya kurejea nchini kitawakaribisha Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Aprili 14, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Gomez aliliambia gazeti hili mashindano yote wanayoshiriki ni muhimu na amekiandaa kikosi chake kupambana kusaka ushindi katika kila mechi watakayocheza.

Kocha huyo alisema wanahitaji kuendelea kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa hivyo ushindi kwenye mechi za ligi ya nyumbani utawaongezea nguvu ya kupambana na kufanya vizuri katika kila hatua.

"Tunahitaji kufanya vizuri katika kila shindano, tumetinga hatua ya robo fainali katika Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini bado tuna jukumu la lufanya vizuri kwenye Kombe la FA na Ligi Kuu ya Tanzania, hayo ndio malengo yetu," alisema kocha huyo raia wa Ufaransa.

Aliongeza morali waliyonayo wachezaji wake kupitia michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, inampa matumaini ya kuendelea kupata matokeo chanya katika michezo itakayofuata.

"Hatutajamaliza kazi, bado msimu haujamalizika, naweza kusema safari inaelekea mwisho lakini hatujaimaliza, tunahitaji kuendelea kujituma ili tufikie malengo ya kila mmoja wetu," Gomes alisema.

Baada ya mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba itasafiri kwenda Shinyanga kuwafuata Mwadui FC katika mechi itakayochezwa Aprili 18, mwaka huu na siku tatu baadaye itakuwa Bukoba kuwavaa wenyeji Kagera Sugar na Aprili 24, mwaka huu itawafuata Gwambina FC.

Habari Kubwa