Gomes kurejea leo kuisuka Simba SC

11Jun 2021
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
Gomes kurejea leo kuisuka Simba SC

​​​​​​​KOCHA Mkuu wa Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba,  Didier Gomes anatarajiwa kurejea leo nchini akitokea kwao Ufaransa kwa mapumziko mafupi, tayari kwa ajili kukiongoza kikosi chake kuelekea mechi za Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.

Didier Gomes.

Akizungumza na gazeti hili jijini jana, Meneja Mkuu wa Klabu hiyo, Patrick Rweyemamu, alisema Gomes atawasili leo muda wowote kwa ajili ya kuendelea na majukumu yake ili kuiwezesha timu hiyo kuweza kutetea mataji yao, Ligi Kuu na Kombe la FA.

“Kocha wetu anatarajiwa kuwasili hapa nchini kesho (leo), muda wowote kuendelea na majukumu ya kuinoa timu yetu ambayo inajiandaa na michezo ya Ligi Kuu pamoja na nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam,” alisema Rweyemamu.

Meneja huyo alisema timu yao inaendelea na mazoezi ikiwa na wachezaji ambao hawajaitwa katika timu zao za taifa.

Mbali na kutinga nusu fainali ya Kombe la FA, pia Simba inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 67, sita mbele ya Yanga inayoshika nafasi ya pili na ikiwa mbele michezo miwili.

Habari Kubwa