Grealish aweka rekodi mpya akitua Man City

06Aug 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Grealish aweka rekodi mpya akitua Man City
  • ***Ni baada ya kukubali kuondoka Aston Villa na kujiunga na miamba hiyo ya Etihad kwa...

JACK Grealish ataweka historia ya kuwa mchezaji wa kwanza Muingereza kulipiwa ada ya uhamisho kiasi cha pauni milioni 100, baada ya kukubali kuondoka Aston Villa, kwenda Manchester City.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 25, jana alitarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kujiunga rasmi na Man City ndani ya saa 24 zijazo na kusaini mkataba wa miaka mitano.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu England wamevunja rekodi ya uhamisho kwenye soka la Uingereza, baada ya wiki iliyopita kuthibitisha kwamba wamekubali kufikia ada inayotakiwa kuipata hudumya ya Grealish.

Mwandisi wa Sportsmail, Chris Wheeler, Machi mwaka huu aliripoti kwamba, City wana nafasi kubwa ya kumsajili Grealish kipindi hiki cha majira ya joto.

Matt Hughes, alibainisha Mei mwaka huu kwamba, City watakuwa tayari kulipa kiasi cha pauni milioni 100, kwa ajili ya kumsajili Grealish.

Na Juni, Daily Mail ikaripoti kuwa City wapo tayari kutoa pauni milioni 100 kwa ajili ya kumsajili Grealish, licha ya Villa kumpa ofa ya mkataba mpya.

Na kama kiungo huyo wa kimataifa wa England atakamilisha dili hilo ndani ya wakati, ana nafasi ya kuichezea Man City kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Leicester City kesho, Jumamosi.

Grealish sasa amevunja rekodi ya pauni milioni 89, ambayo ilitolewa na Manchester United wakati walipomsajili tena kiungo wa Ufaransa, Paul Pogba akitokea Juventus mwaka 2016.

Nyota huyo alirejea kwenye kikosi cha Aston Villa mara baada ya kumalizika likizo baada ya michuano ya Euro 2020 akiwa na England.

Villa walikuwa kwenye mpango wa kumpa ofa mpya Grealish, ambapo walipanga kumpa mshahara wa pauni 200,000 kwa wiki.