Guardiola aridhishwa na kiwango cha City

09Dec 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Guardiola aridhishwa na kiwango cha City

PEP Guardiola amesisitiza ameridhishwa na kazi iliyofanywa na Manchester City kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, licha ya kufungwa 2-1 na RB Leipzig, juzi.

City walisafiri kwenda kwenye Uwanja wa Red Bull Arena Jumanne wakiwa hawajapoteza mechi 14 dhidi ya timu za Ujerumani kwenye mashindano hayo, lakini walijikuta wakifungwa bao la kipindi cha kwanza na Dominik Szoboszlai.

Halafu Andre Silva akaongeza la pili kwa wenyeji kabla ya Riyad Mahrez kuifungia City la kufutia machozi, huku Kyle Walker akitolewa nje kwa kadi nyekundu.

Kikosi hicho cha kocha Guardiola kilishindwa kupindua matokeo hayo, huku wakiwa tayari wamejihakikishia nafasi ya kufuzu hatua ya mtoano kwenye Kundi A.

Pamoja na matokeo hayo, Guardiola alionyeshwa kuridhishwa na matokeo hayo na kazi kubwa iliyofanywa na timu yake.
"Kwenye kipindi cha kwanza tulikosa utulivu, tulikuwa na matatizo ya kuunganisha timu na wao walikuwa na timu nzuri– tulijua kabla ya hatua ya makundi," alisema Guardiola akiwaambia waandishi wa habari.

"Kipindi cha pili kilikuwa bora zaidi, lakini bahati mbaya tulifanya kosa moja au mawili na tukaadhibiwa.

"Tulicheza vizuri sana kipindi cha pili. Tulikuwa na nafasi nzuri ya kupata ushindi, lakini tukapotezwa. Hongera kwa Leipzig.”

Habari Kubwa