Guardiola: Kiwango City hakijashuka misimu sita

30Nov 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Guardiola: Kiwango City hakijashuka misimu sita

PEP Guardiola amesema ni jambo la kujivunia kwamba, kiwango cha Manchester City hakijashuka kwa muda wa
misimu sita mfululizo wakati timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya West Ham juzi, Jumapili.

City waliifunga Everton mabao 3-0 Jumapili iliyopita kwenye Ligi Kuu kabla ya kuifunga Paris Saint-Germain kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano na siku nne baadaye wakawafumua West Ham.

Ilkay Gundogan alifunga bao la ufunguzi kwa wenyeji hao pale kwenye Uwanja wa Etihad ambao ulijaa barafu, huku Fernandinho aliyetokea benchi akifunga la pili na Manuel Lanzini akiwapa la kufutia machozi West Ham.

City, ambao sasa wamecheza mechi saba bila kuruhusu nyavu zao kutikiswa katika mechi nane zilizopita za Ligi Kuu nyumbani, imeshinda 10 kati ya 11 ilizokutana na West Ham.

Baada ya matokeo mengine ya kuridhisha, Guardiola alisifia kazi nzuri ya kikosi chake ambacho anaamini kushinda ndio sehemu ya mtindo wao wa uchezaji.

“Tulitengeneza nafasi nyingi dhidi yao, lakini la msingi ni kwamba tulipata pointi zote tatu,” alisema Guardiola akiiambia
BBC Sport.

“Dakika 15 hadi 20 za mwisho zilikuwa ngumu kucheza, lakini baada ya mchezo dhidi ya PSG tulijifunza kupambana kwa nguvu hadi dakika za mwisho, na hakika yalikuwa matokeo mazuri kwa upande wetu.

“Taji la Ligi Kuu England mara zote ndilo muhimu zaidi na ndio maana kila timu inacheza kwa kupambana kweli kweli.

“Baada ya kushinda mara tatu taji la Ligi Kuu kwa kipindi cha miaka minne iliyopita, ni rahisi tena kuwa kwenye nafasi
ya kuliwania, kiwango chetu kimeendelea kuwa bora na hilo ni muhimu sana kwetu.”

Habari Kubwa