Gyan amfungua mdomo Aussems

06Jan 2019
Isaac Kijoti
Zanzibar
Nipashe Jumapili
Gyan amfungua mdomo Aussems

KIWANGO cha juu kilichoonyeshwa na beki wa pembeni wa kimataifa wa Simba, Mghana, Nicholas Gyan, katika mechi ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Chipukizi United ya Pemba, kimemkuna Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems.

Beki wa pembeni wa kimataifa wa Simba, Mghana, Nicholas Gyan

Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amaan juzi usiku, Gyan alihusika katika mabao matatu wakati Simba ikiibuka na ushindi wa magoli 4-1.

Pasi ya mwisho ya mabao mawili yaliyofungwa na Meddie Kagere dakika ya 32 na 59, zilitoka kwa Gyan huku akiifungia timu yake kwa kichwa bao la pili dakika ya 55.

Akizungumza na Nipashe mara baada ya mechi hiyo, Aussems alisema Gyan alikuwa kwenye kiwango cha juu na kumtaka kuendeleza moto huo katika mechi zijazo.

"Ni kiwango cha juu kwa Gyan, leo amefunga na kutoa pasi za mwisho," alisema na kutania, 'huenda anaweza kuwa kipa mzuri pia'.

"Lakini pia timu ilicheza vizuri, ingawa tulipaswa kufunga mabao mengi zaidi kutokana na nafasi tulizotengeneza."

Katika mechi hiyo bao la Chipukizi lilifungwa na Godwin Kiongozi na kufanya ubao wa matangazo uwanjani hapo kusomeka 1-1 kabla ya dakika ya 55 Gyan kuifungia Simba bao la pili.

Kagere aliiandikia Simba bao la tatu kabla ya nahodha, John Bocco kufunga la nne kwa mkwaju wa penalti kufuatia Rashid Juma kuchezewa madhambi ndani ya 18.

Simba iliyopo Kundi B, itashuka tena uwanjani leo usiku kuvaana na KMKM kabla ya kuhitimisha hatua ya makundi na Mlandege wiki ijayo.

Habari Kubwa