Haaland aweka rekodi mpya Bundesliga

29Nov 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Haaland aweka rekodi mpya Bundesliga

ERLING Haaland alihitaji dakika saba kufunga akitoka kuuguza majeraha yake na kufikisha bao la 50 kwenye Ligi Kuu Ujerumani, Bundesliga, juzi Jumamosi.

Kabla ya kurudi uwanjani, Halaand, alikuwa nje ya dimba tangu Oktoba kutokana na maumivu ya misuli.

Halaand alifunga bao hilo akitokea benchi na kuweka rekodi mpya ya kuwa mchezaji kijana zaidi kufikia mabao hayo kwenye ligi hiyo, wakati Borussia Dortmund ikitoka nyuma na kuifumua Wolfsburg 3-1.

Nyota huyo wa kimataifa wa Norway amefikisha idadi ya mabao 50 akiwa na umri wa miaka 21 na siku 129, na kumfanya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufikisha idadi hiyo kwenye historia ya Bundesliga.

Wout Weghorst alianza kuwapa Wolfsburg bao la uongozi kabla ya penalti ya Emre Can na Donyell Malen kupindua matokeo na Haaland kufunga la tatu.

Dortmund ilipaa kileleni mwa msimamo kwa muda, lakini Bayern Munich iliwachapa Arminia Bielefeld bao 1-0 na kurudi kileleni.

Bao hilo pekee lilifungwa na Leroy Sane kwa shuti kali nje ya boksi la penalti.

Bayern Munich sasa imefikisha mabao 102 kwenye Bundesliga kwa mwaka 2021, wakiivunja ile ya Cologne ya kufunga mabao 101 mwaka 1977.

Bao hilo la Haaland lilimfanya kufikisha mabao 10 kwenye Ligi Kuu aliyoifungia Dortmund kwenye mechi saba msimu huu.

Habari Kubwa