Harmorapa: 'Seduce Me' hautafunika 'Ajitokeze'

31Aug 2017
Beatrice Shayo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Harmorapa: 'Seduce Me' hautafunika 'Ajitokeze'

MSANII wa Bongo Fleva, Harmorapa amesema wimbo wake mpya aliyouachia unaojulikana kwa jina la 'Ajitokeze' anaamini hauwezi kufunikwa na staa wa Bongo Fleva, Ally Saleh 'Ali Kiba' licha ya kwamba ametoa kibao kikali cha 'Seduce Me'.

MSANII wa Bongo Fleva, Harmorapa.

Harmorapa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wimbo wake mpya ambao ameuachia wiki iliyopita.

Alisema wimbo huo mpya siku anauachia kuingia mtaani umepishana saa chache na kibao kipya cha Seduce, hivyo haamini kama unaweza kufunikwa huku pia akibainisha labda kwa kuwa kila mmoja ana mashabiki wake.

“Ali Kiba kama Ali Kiba, atabaki kuwa Ali Kiba na nyimbo zake ni nzuri na amekuwa anafanya vizuri katika 'game' la muziki.

Muziki wake utadumu kwa kuwa ngoma yake ni kubwa ila siwezi kusema kuwa kutoka kwa ngoma yake kutaifanya ngoma yangu kuwekwa kapuni, kila mmoja ana kiwango chake, yeye ana mashabiki wake na mimi nina wangu,” alisema.

Aidha, alisema wimbo huo mpya unazungumzia maisha halisi aliyoyapitia na kuhusu jamii kwa ujumla, hivyo anaamini mashabiki wake watafurahia kibao hicho.

“Huu wimbo unamaanisha kuwa sijaona mtu anayezungumziwa mitaani kama mimi, ndio maana nikauita jina la 'Ajitokeze' na wiki ijayo ninatarajia kutoa video yake ambayo ipo vizuri na mashabiki wataifurahia,” alisema Harmorapa.

Harmorapa alisema mpaka sasa ana jumla ya nyimbo nne alizoziachia ambazo ni 'Usigawe Pasi, Kiboko ya Mabishoo, Nundu na Ajitokeze'.