Hatima uchaguzi Yanga wiki ijayo

16Jan 2019
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Hatima uchaguzi Yanga wiki ijayo
  • Waliofungua kesi mahakamani wakubali kuzifuta, kasoro kufanyiwa kazi TFF

UCHAGUZI wa klabu ya Yanga uliozuiliwa mahakamani kufuatia baadhi ya wanachama kufungua kesi kupinga mchakato wake, sasa utafanyika baada ya siku saba kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF) Ally Mchungahela.

Ijumaa iliyopita Mchungahela alitangaza kuusogeza mbele uchaguzi huo ambao ulikuwa ufanyike Jumapili iliyopita kutokana na wanachama hao kufungua kesi mahakamani kuzuia uchaguzi huo.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam,Mchungahela alisema kuwa baada ya kutangaza kuuahirisha uchaguzi huo Kamati ilitumia njia mbalimbali kuwafikia wale wote waliofungua kesi ili kujua msingi wa malalamiko yao na uhalali wao kusimama mahakamani dhidi ya Klabu hiyo ya Yanga kwa mujibu wa Katiba ya Yanga.  

“Tumejiridhisha kuwa malalamiko yote yamejikita kwenye maeneo makuu matatu mosi, uhalali wa wanachama wenye kadi za zamani, kadi za CRDB na kadi za Benki ya Posta kupiga kura, pili kukataliwa majina ya wanachama katika baadhi ya matawi ya Yanga kuingizwa kwenye rejista ya wanachama wa Yanga, na tatu sintofahamu ya nafasi ya Mwenyekiti wa Yanga hivyo kusababisha baadhi ya wanachama wenye sifa za uongozi, kuwa na mashaka kujitokeza”, alisema Mchungahela.

Alisema kamati hiyo imebaini wanachama waliofungua kesi ukimuondoa mmoja si wanachama hai wa Yanga.

“Kati ya wanachama waliofungua keshi, ni mwanachama mmoja tu ambaye ndio anasifa ya kuwa mwanachama wa klabu hiyo, lakini pia kamati tumewapelekea walalamikaji wote kuwa uanachama wao Yanga una hitilafu ki-Katiba, hivyo hawakuwa na sifa kupeleka malalamiko yao popote pale kwa kivuli cha uanachama wa klabu hiyo lakini pia Katiba za Yanga, TFF, CAF na FIFA haziruhusu wanachama wao kupeleka malalamiko mahakamani, hivyo utaratibu huo hauna tija mbali na kuiondolea klabu sifa ya kuheshimu taratibu, malalamiko yao yote waliyoainisha yanatatulika kwa taratibu zilizopo ndani ya shirikisho, hivyo hawana budi kuondoa kesi hizo mahakamani mara moja,” alisema Mchungahela

Alisema walalamikaji wote waliopeleka kesi mahakamani wamekubaliana nao na wamekubali kuondoa kesi mahakamani na kuruhusu kamati kuwasilisha malalamiko yao TFF ili yafanyiwe kazi ndani ya siku saba kuanzia juzi.

“Naomba niwahakikishie wanachama wa Yanga, ratiba ya uchaguzi huo mdogo tutaitoa baada ya siku saba kuanzia juzi,” alisema Mchungahela.

Alisema pia wanachama wanapaswa kufahamu uchaguzi huo mdogo ni kwa ajili ya kujaza nafasi zilizowazi na viongozi watakaopatikana watakaa madarakani kwa kipindi cha mwaka mmoja kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu.

Waliopitishwa kugombea uongozi kabla ya uchaguzi kusimamishwa kwa upande wa mwenyekiti ni Dk. Jonas Tiboroha, Baraka Igangula na Yono Kave

Habari Kubwa