Hatma Mbao, Mbeya City Ligi Kuu Bara leo

01Aug 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Hatma Mbao, Mbeya City Ligi Kuu Bara leo

TIMU za Mbao FC na Mbeya City, leo zinatarajia kujua hatma yao ya kubaki kwenye Ligi Kuu au kushuka daraja, zitakapocheza mechi za marejeano za mchujo kwenye viwanja vyao vya nyumbani.

Mbao FC itakuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani, CCM Kirumba mjini Mwanza kuikaribisha Ihefu FC katika mechi ambayo itakuwa inaangaliwa zaidi na mashabiki wengi wa soka nchini.

Kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Geita Gold kutoka mkoani Mwanza.

Jumatano iliyopita kwenye mechi za awali, Mbao FC ilikiona cha moto, ilipochapwa mabao 2-0 dhidi ya Ihefu FC kwenye Uwanja wa Highland Estate, Mbalizi, Mbarali mkoani Mbeya.

Kwa matokeo hayo, Mbao ina kazi kubwa ya kufanya, kupata ushindi wa kuanzia mabao 3-0 ili kuwa na uhakika wa kuendelea kubaki Ligi Kuu, vinginevyo msimu ujao itacheza Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.

"Wao walishinda kwao na sisi tunawakaribisha kwetu Mwanza, haitokuwa mechi rahisi kwao, tutawapa wakati mgumu sana," alisema Waziri Junior, kinara wa mabao wa timu hiyo akiwa amemaliza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kucheka na nyavu mara 13.

Kocha Mkuu wa Ihefu, Maka Malwisi alisema amejiandaa kikamilifu na mechi ya marudiano na anajua itakuwa ngumu, lakini amewaandaa vijana wake kukabiliana na kila hali.

"Nimeshawandaa vijana wangu kucheza mechi zote mbili, kwa hiyo najua ni jinsi gani na mfumo gani tutacheza," alisema kocha huyo.

Timu ya Mbeya City yenyewe italazimika kupata ushindi wa aina yoyote ile ili kubaki Ligi Kuu kwani katika mechi ya mwanzo Jumatano iliyopita, ililazimishwa sare ya bao 1-1 ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Sekondari ya Nyankungu mjini Geita.

Ihefu FC ilishika nafasi ya pili kwenye Kundi A, huku Geita nayo ikimaliza katika nafasi kama hiyo kwa upande wa Kundi B, wakati Mbeya City, ikishika nafasi ya 15 na Mbao FC ya 16 kwenye Ligi Kuu Bara, hivyo timu zitakazopata matokeo ya jumla zitaungana na zingine 16 kushiriki Ligi Kuu msimu ujao.

Habari Kubwa