Hesabu za ubingwa Yanga sasa nyepesi

06May 2016
Faustine Feliciane
Nipashe
Hesabu za ubingwa Yanga sasa nyepesi
  • ***Ni baada ya washindani wao wa karibu Azam FC kupokwa pointi tatu kwa kosa la kumchezesha mchezaji aliyekuwa na kadi tatu za njano...

MABINGWA watetezi Yanga, wanaweza kutawazwa taji Ligi Kuu Bara msimu huu bila kushuka dimbani kama walivyofanya Leicester City ya England, lakini tu iwapo mahasimu wao, Simba watapoteza mechi dhidi ya Mwadui FC Jumapili wiki hii.

YANGA

Mabingwa hao wapya wa England walitwaa taji kwa mara ya kwanza katika historia Jumatatu wiki hii bila kushuka dimbani, baada ya washindani wao wa karibu, Tottenham kushindwa kuifunga Chelsea ili kuizuia timu hiyo ya kocha Claudio Ranieri kutwaa taji mapema.

Mahesabu ya Yanga kusogea jirani zaidi na kutetea taji lao, yaliongezeka jana baada ya waliokuwa washindani wao wa karibu, Azam FC kupokwa pointi tatu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

TFF imeikata Azam pointi hizo na mabao matatu baada ya kubainika kumtumia kimakosa beki Erasto Nyoni kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City, Septemba 27, wakati mchezaji huyo alikuwa na kadi tatu za njano. Katika mechi hiyo Azam walishinda mabao 2-1.

Kutokana na kukatwa pointi hizo, mshindani wa karibu kwenye mbio za ubingwa anabaki kuwa Simba, ambao sasa wamepanda hadi nafasi ya pili ya msimamo, huku Azam wakishuka hadi nafasi ya tatu wakiwa na pointi 57 kutoka 60 walizokuwa nazo awali kabla ya punguzo hilo.

Hiyo ina maana kuwa, hata kama Azam watashinda mechi tatu zilizobaki watafikisha pointi 66, ambazo tayari Yanga wameshazikusanya.

Simba yenye pointi 58, inaweza kufikisha pointi 70 kama watashinda mechi zao nne zilizobaki.
Ili Yanga kutwaa taji bila kushuka dimbani, wataomba Simba wapoteze mchezo wao, hivyo kuandika rekodi ya kutetea taji wakiwa na mechi tatu mkononi.

Lakini hata kama Simba watashinda mechi hiyo, Yanga wanaweza kutwaa ubingwa iwapo wataifunga Mbeya City Jumanne ijayo.

Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari TFF, Alfred Lucas, uamuzi wa kuipoka pointi Azam ulifikiwa kwa mujibu wa kanuni ya 14, kifungu kidogo cha 37 kinachoeleza adhabu itakayotolewa kwa timu iliyochezesha mchezaji mwenye kadi tatu za njano.

"Azam wamevunja kanuni ya 37 kifungu kidogo cha nne, ambacho kinaelezea mchezaji atakayechezeshwa akiwa na kadi tatu za njano, timu yake itakumbana na adhabu hiyo," alisema Lucas.

Hata hivyo, alipotafutwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawembwa alisema hana taarifa za uamuzi huo wa TFF.
"Siwezi kuzungumza lolote kwa sasa kwa sababu sina taarifa za uamuzi huo wa TFF," alisema bosi huyo wa Azam.

Habari Kubwa