Hii ndiyo Yanga bhana

14Feb 2016
Faustine Feliciane
Nipashe Jumapili
Hii ndiyo Yanga bhana
  • ***Yasafiri katika mazingira magumu, lakini yarejea na ushindi kutoka ugenini Mauritius

LICHA ya safari yao ya kuelekea Mauritius kukumbwa na vikwazo,ikiwa ni pamoja na kukwama Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Kambarage Nyerere, Dar es Salaam kwa zaidi ya saa 10 siku moja kabla ya mchezo, Yanga jana ilifanya kweli baada ya kuibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Cercle de Joachim.

WACHEZAJI WA YANGA

Shujaa wa Yanga kwenye mechi hiyo alikuwa mshambuliaji Donald Ngoma aliyefunga bao pekee baada ya kazi nzuri ya Juma Abdul.

Matokeo hayo yanawapa nafuu Yanga kwenye mechi ya marudiano wiki mbili zijazo, kwani sasa watahitaji sare ya aina yoyote kusonga mbele.

Iwapo watafuzu kwa hatua ya pili, mabingwa hao wa Bara watakumbana na timu ya APR ya Rwanda au Mbabane Swallows ya Swaziland.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi, Hubert Marie Bruno Andriamiharisoa kutoka Madagascar, Yanga ilipata pigo kipindi cha pili, baada ya mpishi wa bao lake, Juma Abdul kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ilichukuliwa na Pato Ngonyani aliyemalizia vizuri.

Yanga ilitarajiwa kugeuza jana baada ya mchezo huo na itaelekea moja kwa moja Pemba kuweka kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa.
Kikosi cha Yanga kwenye mchezo huo

Ally Mustafa 'Barthez', Juma Abdul/Pato Ngonyani (dk70), Oscar Joshua, Kelvin Yondan, Vincent Bossou, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Amissi Tambwe/Paul Nonga (dk68) na Deus Kaseke.

Wakati Yanga wakianza vyema michuano hiyo, hapa nyumbani timu ya Mafunzo ya Zanzibar imejiweka katika mazingira magumu ya kusonga mbele baada ya kukubali kipigo cha magoli 3-0 kutoka AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Magoli hayo ya kipindi cha kwanza kwenye Uwanja wa Aman mjini Zanzibar yameiweka kwenye wakati mgumu, kwani sasa wanatakiwa kushinda mabao 4-0 ili kusonga mbele.

Habari Kubwa