Hitimana anogewa kufundisha Bongo

21Nov 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Hitimana anogewa kufundisha Bongo

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Namungo FC, Mnyarwanda, Hitimana Thiery, amesema anapenda kuendelea kufanya kazi hapa nchini kutokana kuwa na Ligi Kuu bora na yenye kushirikisha timu zenye ushindani.

Hitimana ambaye aliachana rasmi na Namungo hapo juzi, alisema tayari ameanza mazungumzo na baadhi ya timu zilizoko kwao Rwanda, lakini anatoa kipaumbele kwa timu za Tanzania.

"Nakwenda nyumbani Rwanda kwa ajili ya mapumziko, nasikia pia kuna timu inanihitaji huko kwetu, nitakwenda kuisikiliza, lakini mimi ningependa sana kufundisha Tanzania kwa sababu kuna ligi bora, pamoja na timu zenye ushindani sana, hii inatujenga hata sisi makocha kila siku tunaumiza vichwa na kujifunza vitu vipya," alisema Hitimana.

Taarifa zilizopatikana jijini zinasema Hitimana anawindwa na klabu ya Mbeya City ambayo hivi karibuni pia ilitangaza kuachana na kocha wake mkuu, Amri Said.

Kwa sasa Mbeya City iko chini ya Kocha Msaidizi, Mathias Wandiba na imeelezwa mmoja wa makocha waliopendekezwa kutua klabuni hapo ni Hitimana.

Hitimana aliiongoza vyema Namungo katika msimu uliopita na ameipatia tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Habari Kubwa