Hitimana Kocha Mkuu Simba CAF, Gomes msaidizi

11Sep 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Hitimana Kocha Mkuu Simba CAF, Gomes msaidizi
  • ***Aibwaga Mtibwa, asaini rasmi mwaka mmoja Msimbazi, kwenye Ligi Kuu Mfaransa kuwa kocha mkuu, huku Matola...

BAADA ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), kutaja orodha ya makocha ambao hawana sifa ya kuziongoza timu zao kweye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika kuanzia msimu huu, huku Kocha Mkuu wa Simba,
Mfaransa Didier Gomes, akiwa miongoni mwao, haraka klabu hiyo ...

imechukua hatua stahiki kufanikiwa kumrejesha katika benchi la timu hiyo, imefahamika.

CAF juzi ilitangaza kuwa kuanzia msimu huu kocha mkuu anapaswa kuwa na Leseni ya UEFA A Pro ambayo ni sawa na Caf A, huku makocha wasaidizi wakipaswa kuwa na Leseni B, jambo ambalo makocha wote wa Simba, Kocha Mkuu, Gomes anakosa sifa hiyo huku pia Msaidizi wake, Selemani Matola naye akikosa sifa katika nafasi yake.

Hata hivyo, haraka bila kupoteza muda uongozi wa Klabu ya Simba ukaonyesha umakini wake kwa kuhakikisha inafanya mazungumzo na kumsainisha Thierry Hitimana mkataba wa mwaka mmoja ili kuja kusimama kama kocha mkuu wa timu hiyo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Gomes atakuwa akibeba jukumu la kocha msaidizi.

Gomes ambaye leseni yake ni UEFA Diploma A, daraja hilo linamruhusu kuwa kocha msaidizi katika michuano hiyo ya CAF, lakini kwa upande wa Ligi Kuu anakidhi vigezo vya kuwa kocha mkuu, hivyo katika mechi za ndani ataendelea na jukumu lake la ukocha mkuu ambapo sasa atakuwa akisaidiwa na Hitimana pamoja na Matola.

Hitimana mwenye Leseni A ya CAF, daraja ambalo linamruhusu kuwa kocha mkuu kwenye michuano ya shirikisho hilo na mingine nchini, alikuwa asaini mkataba na Mtibwa Sugar, lakini jana aliikacha ofa hiyo na kwenda kumwaga wino Simba baada ya kutangaziwa dau nono zaidi.

Sheria mpya ambayo inaanza msimu huu inataka kocha ambaye anatoka ndani ya Afrika lazima awe na Leseni ya CAF A na kwa makocha ambao wanatoka nje ya Afrika kwa Bara la Ulaya wawe na Uefa A Pro.

Taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili jijini jana kutoka chanzo chetu ndani ya Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, tayari klabu hiyo imemalizana na Hitimana, ambaye anakidhi vigezo kwa kuwa na leseni ya CAF A, na sasa atakuwa akisaidiwa na Gomes kwenye michuano hiyo ya kimataifa.

"Katika kuimarisha benchi la ufundi, tumempa mkataba wa mwaka mmoja kwa ajili ya kusaidiana na Gomes na Matola, kuelekea michuano ya kimataifa," alisema mjumbe mmoja kutoka kwenye bodi hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa si msemaji katika suala hilo.

Gazeti hili lilimtafuta Hitimana, ambaye alikiri kumalizana na uongozi wa Simba kwa mkataba wa mwaka mmoja kwenda kuwa sehemu ya benchi la ufundi la timu hiyo kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.

"Ni kweli nilikuwa na mazungumzo na viongozi wa Simba na tayari nimesaini mwaka mmoja, makubaliano mengi ni baada ya nusu msimu tutakaa na kuzungumza kuhusu kuongeza mkataba mwingine," alisema Hitimana.

Kuhusu Mtibwa Sugar, alisema hadi anarejea Tanzania, alikuwa na makubaliano ya kuja kuinoa timu hiyo, lakini Simba wamefanikiwa kumpa ofa nzuri ambayo imezidi ile ya mwajiri wake wa zamani, 'Wakata Miwa' hao.

Kwa upande wa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema viongozi wa klabu hiyo wako makini na wanatambua suala la kanuni na sheria za CAF na wamejipanga katika hilo.

"Tulishajua na si suala la 'suprise' kwetu, tumejiandaa vizuri na tunawahakikishia mashabiki wa Simba wasubiri hadi Januari na Kocha Gomes atakuwa sehemu ya benchi la ufundi la Simba," alisema Kamwaga.