Igangula aiomba serikali kuingilia uchaguzi Yanga

13Jan 2019
Renatha Msungu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Igangula aiomba serikali kuingilia uchaguzi Yanga

MGOMBEA wa nafasi ya Mwenyekiti katika uchaguzi mdogo wa Yanga, Mbaraka Igangula ameiomba Serikali kuingilia kati mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo ambao umesimamishwa hadi hapo itakapotangazwa baadaye.

Uchaguzi huo mdogo wa Yanga ulipangwa kufanyika leo, lakini juzi mchana lilitolewa tangazo la kusimamishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Malangwe Mchungahela.

Akizungumza na gazeti hili jana, Igangula alisema kuwa ili Yanga iweze kupata viongozi wake ni lazima serikali itoe tamko ambalo litasaidia kumaliza "vigisuvigisu" zinazofanywa na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo ambao hawataki kuwapo kwa uchaguzi. Igangula alisema kuwa wanachama wachache ndio wanaozuia kuwapo kwa uchaguzi jambo ambalo linaigharimu klabu yao kwa kushindwa kufanya mambo ya maendeleo.

"Kuna kila haja ya Serikali kuweka mkono wake, kwa sababu kuna wanachama wachache ... ambao wanaijaribu na wanania ya kuia klabu ya Yanga," alisema Igangula.

Mgombea huyo aliongeza kuwa makundi yaliyopo katika klabu hiyo pia yanachangia kuvuruga mchakato wa uchaguzi kila wanapotakiwa kufanya hivyo.

Hata hivyo Igangula aliongeza kuwa ataendelea kuipigania Yanga kwa sababu yeye ni mwanachama na alishawahi kuiongoza klabu hiyo miaka ya nyuma.

"Wengi tunahitaji kuona Yanga inasonga mbele na kusimama imara kama ilivyokuwa zamani, ila kuna wanachama wachache wanataka kukwamisha malengo haya, lengo kuu tulilonalo ni kuona tunasonga mbele na si kurudi nyuma," Igangula aliongeza.

Aliwakumbusha wanachama kuhakikisha wanachagua viongozi ambao watakuwa ni waadilifu na si kuchagua bora kiongozi ili kuepusha kuirudisha nyuma klabu yao.

"Uamuzi wa kuahirisha uchaguzi ndio kunatupa nguvu ya kusonga mbele katika kampeni zetu, ninaamini tutashinda na kuifanya Yanga iwe yenye kuheshimika," alisema Igangula.

Habari Kubwa