Igangula awasuta viongozi Yanga

08May 2016
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Igangula awasuta viongozi Yanga

ALIYEKUWA mwenyekiti wa Yanga, Mbaraka Igangula amewataka wanachama wa klabu hiyo kuchagua viongozi watendaji na kuacha wale wanaoendelea 'kunadi' ramani za uwanja badala ya kuanza ujenzi kwa miaka 14 sasa.

Yanga inatarajia kufanya uchaguzi mkuu wake Juni 26 jijini Dar es Salaam kwa kutumia katiba ya mwaka 2010 pamoja na kadi za wanachama za zamani.

Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Igangula alisema kuwa anashangazwa kuona ujenzi wa uwanja huo bado haujaanza na kila siku viongozi walioko madarakani wanaonyesha ramani tofauti.

Igangula aliwataka wanachama wa Yanga kuwa makini kwenye uchaguzi huo ili wapate viongozi watakaoiletea heshima na hadhi inayolingana na klabu yao.

"Wakati namkabidhi Kifukwe (Francis) madaraka 2002 nilimpa na ramani ya uwanja, lakini hadi leo bado tunaendelea kuonyeshwa ramani tofauti za uwanja utakavyokuwa, jambo la ajabu hili," alisema Igangula ambaye ni mhandisi.

Hata hivyo Igangula alisema kuwa hawezi kugombea nafasi yoyote katika uchaguzi huo kwa sababu yeye ni mmoja wa viongozi wa Shirikisho la Wafanyakazi nchini (TUCTA).

Mchakato wa uchaguzi huo unaosimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) utaanza Mei 26 kwa wanachama kuchukua fomu wakati kampeni kwa wagombea waliopitishwa zitaanza Juni Mosi hadi 4.

Habari Kubwa