IMOOOO...Yanga yabisha hodi nusu fainali CAF

14Aug 2016
Mahmoud Zubeiry
Lete Raha
IMOOOO...Yanga yabisha hodi nusu fainali CAF

YANGA bado imo kwenye mashindano. Kikosi hicho kimeanza kutakatisha njia kwa kufufua matumaini ya kuelekea Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika,

Winga wa Yanga Simon Msuva, akiruka kumiliki mpira wakati wa mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi yao na Mo Bejaia kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam

baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mouloudia Olympique Bejaia ya Algeria katika mchezo wa marudiano Kundi A Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Shujaa wa Yanga katika mchezo huo wa jana alikuwa Mrundi Amissi Tambwe, aliyefunga bao hilo pekee kipindi cha kwanza na sasa timu hiyo imefikisha pointi nne baada ya awali kufungwa mechi tatu na kutoa sare moja, lakini pamoja na matumaini hayo inaendelea kushika mkia katika Kundi A.

TP Mazembe inaendelea kuongoza Kundi A kwa pointi zake 10 baada ya mechi nne, ikishinda tatu na kutoa sare moja, ikifuatiwa na Bejaia na Medeama, ambazo kila moja ina pointi tano kutokana na sare mbili na ushindi mmoja.

Tambwe alifunga bao hilo dakika ya pili tu ya mchezo, akimalizia mpira uliookolewa kufuatia Simon Msuva kuunganisha kwa kichwa krosi ya Juma Abdul kutoka upande wa kulia.

Ili Yanga ifuzu hatua ya nusu fainali, haina budi kuiomba Medeama ya Ghana ifungwe na TP Mazembe leo na baadaye katika mechi yake ya mwisho itoke sare na MO Bejaia, huku vijana wa Kocha Mholanzi Hans van der Pluijm wakishinda mchezo wake wa ugenini dhidi ya Mazembe.

Yanga ingeweza kuondoka na ushindi mnono jana, kama mshambuliaji wake, Obrey Chirwa angekuwa makini na kutumia vizuri nafasi zaidi ya nne za wazi alizotengenezewa.

Nafasi iliyowasikitisha zaidi mashabiki wa Yanga ni ya kipindi cha pili, Chirwa aliporuka kichwa cha mkizi baada ya krosi ya Msuva kutoka kushoto, lakini akapiga hewa akiwa amebaki na kipa, huku mpira ukienda nje.

Kocha Pluijm alilazimika kufanya mabadiliko ndani ya robo ya kwanza ya mchezo, baada ya beki wake, Andrew Vincent ‘Dante’ kuumia na kumuingiza mkongwe, Kevin Yondan aliyemalizia vizuri mchezo huo.

Pia alilazimika kumpumzisha beki wake wa kulia, Juma Abdul, baada ya kipindi cha kwanza kupata majeraha nyama za paja na kumuingiza kiungo Said Juma ‘Makapu’ aliyekwenda kucheza kama kiungo wa ulinzi, huku Mbuyu Twite akihamia beki ya kulia.

Yanga itahitimisha mechi zake za Kundi A Kombe la Shirikisho kwa kumenyana na wenyeji TP Mazembe ya DRC mjini Lubumbashi Agosti 23, mwaka huu.

Kikosi cha Yanga SC kilikuwa: Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul/Said Juma ‘Makapu’ dk 46, Mwinyi Mngwali, Andrew Vincent ‘Dante’/Kevin Yondan dk.17, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Obrey Chirwa na Deus Kaseke/Juma Mahadhi.

MO Bejaia: Chamseddine Rahmani, Ismail Benettayeb, Faouzi Rahal, Sofiane Khadir, Soumaila Sidibe, Zakaria Bencherifa, Mohamed Yacine Athmani, Morgan Betorangal, Sofiane Baouali, Amar Benmelouka na Kamel Yesli.

Habari Kubwa