Itakuwa vipi leo Yanga Dar, Simba Shy

07Feb 2016
WAANDISHI WETU
Nipashe Jumapili
Itakuwa vipi leo Yanga Dar, Simba Shy
  • ***Vigogo hao wa soka katika nafasi ya kwanza na pili kwenye msimamo wanawinda ushindi nyumbani na ugenini, huku Azam nao wakirejea uwanjani...

SAFARI ya Yanga kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu inaanza wiki ijayo, lakini kabla kukwea pipa, leo inacheza na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wapinzani wao Simba wenye manukato ya ushindi katika mechi nne mfululizo chini Kocha Jackson Mayanja, wako Shinyanga kwenye Uwanja wa Kambarage kusaka ushindi mwingine dhidi ya Kagera Sugar.
Azam FC baada ya kufanya vizuri na kutwaa taji kwenye mashindano maalum nchini Zambia, leo wanarejea kwenye ligi kwa kupambana na Mwadui FC kwenye Uwanja wa Chamazi.
Azam wako nafasi ya tatu wakiwa na pointi 39 na michezo miwili mkononi na leo wamepania kuanza safari ya kurejea kileleni.
Yanga inakwea pipa Jumatano ijayo kwenda Mauritius kucheza mchezo wake wa awali dhidi Cercle de Joachim.
Lakini kabla ya safari hiyo, Kocha Hans van der Pluijm hataki longolongo, amewaagiza wachezaji wake kuzoa pointi dhidi ya kikosi cha King Abdallah Kibadeni.
Katika mechi tano za mwisho za ligi, Yanga imembulia pointi 10, ikishinda mara tatu, sare moja na kupoteza moja.
moja.
Kipigo cha mabao 2-0 kutoka Coastal Union na sare ya 2-2 na Prisons, kulitibua mipango ya Pluijm kuwakimbia kwa mbali wapinzani wao Simba, ambao sasa wako nyuma kwa tofauti ya pointi moja tu.
"Tunahitaji ushindi kwenye mchezo wa kesho (leo), lakini pia nisingependa wachezaji wangu wahatarishe afya zao, nataka wacheze kwa umakini ili kuepuka majeraha kabla ya kusafiri kwenda Mauritius.
"Hatujafanya vizuri katika mechi mbili za mwisho, tumetoka sare mara moja na kupoteza mchezo mmoja, sasa unaona jinsi ilivyo muhimu kwetu kushinda mechi ya leo," alisema Pluijm
Alisema ushindi utawajengea wachezaji wake ari na dhamira ya kufanya vziuri kwenye mechi yao ya kimataifa Mauritius.
"Ruvu wanacheza soka la nguvu, hata kama hawafanyi vziuri kwenye ligi kwa sasa, lakini hatuwezi kuwabeza.
Siwezi kutabiri matokeo, Yanga ni timu kubwa na mchezo utakuwa mgumu, tumejipanga kupata matokeo mazuri na naamini wao pia wamejipanga hivyo."
Kwenye Uwanja wa Kambarage, Simba wakiwa katika nafasi ya pili na pointi zao 39, wanakipiga na Kagera Sugar.
Wekundu hao wa Msimbazi wanashuka uwanjani wakiwa bado na utamu wa ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya JKT Mgambo, huku Kagera nao wakichekelea ushindi wa 2-1 dhidi ya Majimaji.
Kocha Mayanja alisema jana kuwa anachoangalia mbele kwa sasa ni mwendelezo wa ushindi.
Chini yake, Simba imekusanya pointi 12 katika mechi nne za ushindi dhidi ya Mtibwa (1-0), JKT Ruvu (2-0), African Sports (4-0) na Mgambo JKT (5-1).
Ushindi wa mechi hizo umewafungua vinywa mashabiki wa Simba ambao sasa wanaona timu yao inaweza kutwaa taji, lakini Mayanja anasema safari ni ndefu na hawezi kutoa utabiri kama kasi ya kikosi chake ndiyo kielelezo cha kutwaa taji kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2011/12.
Licha ya Kagera kuwa na mzunguko wa kwanza usio na mafanikio, wana rekodi nzuri za mechi za duru la pili wakishinda mbili mfulilizo kwenye Uwanja wa Kambarage.
Kabla ya kuumana na Simba, Kagera iliyo katika nafasi ya 12 baada ya kukusanya pointi 15, ilizitungua Mbeya City (2-0), kisha Majimaji (2-1).
Kocha Mayanja ambaye sasa anaonekana kama mkombozi Msimbazi, alisema jana kuwa kikosi kinacheza na timu ngumu, lakini kwa sababu dhamira yao ni kushinda mechi zote zilizosalia, hana shaka na ushindi.
“Nimekiandaa vizuri kikosi vizuri, kama wachezaji wangu watafuata maelekezo vziuri, tutashinda mechi hii dhidi ya timu ngumu.
Kocha wa Kagera, Adolf Richard alisema alisema anajivunia rekodi nzuri ya ushindi kwenye Uwanja wa Kambarage tangu kuanza duru la pili, hivyo ana hakika watafanya vizuri kwenye mchezo wa leo.
Mechi nyingine leo hii, Mbeya City watacheza 'dabi' na majirani zao Prisons, wakati Ndanda watakipiga na Mtibwa Sugar, Toto African watakuwa nyumbani kucheza dhidi ya Coastal Union na Majimaji dhidi ya JKT Mgambo.

Imeandikwa na Faustine Feliciane, Adam Fungamwango (Dar) na Lasteck Alfred (Shinyanga).

Habari Kubwa