IWE ISIWE

07Feb 2016
Lete Raha
IWE ISIWE
  • *Yanga yapanga kipigo cha kupandia ndege ya CAF *Simba wapewa mizuka mipya ya ubingwa

KOCHA wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm, amesema matokeo mabaya waliyoyapata katika mechi mbili zilizopita, yameifanya mechi yao ya leo iwe dhidi ya JKT Ruvu ngumu kwa sababu ni lazima washinde ili kujiimarisha katika mbio za ubingwa.

Yanga yenye pointi 40, itaivaa JKT kwenye Uwanja wa Taifa leo ikitokea kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Prisons na kichapo cha 2-0 dhidi ya Coastal Union mjini Tanga na Pluijm anaona kwamba ni lazima wajirekebishe leo kama wanataka kutetea vyema ubingwa wao.
Pluijm amesema, “Tumekuwa na matokeo mabaya kwenye mechi zetu mbili zilizopita. Hivi sasa tunajiandaa na mchezo wa kimataifa wa klabu bingwa dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius, hivyo mchezo wetu dhidi ya JKT Ruvu ni muhimu sisi kushinda kwa gharama yoyote.
“Lazima tuwe na mahali pa kuanzia na hii ni kupata ushindi kwenye ligi. JKT Ruvu ni timu nzuri, lakini lazima tupate pointi tatu kabla hatujapanda ndege.”
Yanga itaondoka Jumatano kuelekea Mauritius kuikabili timu hiyo watakayoivaa wikiendi katika mechi yao ya kwanza ya hatua ya awali ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu Afrika
JKT Ruvu ambayo ilipoteza kwa bao 2-1 dhidi ya Mbeya City Alhamisi iliyopita pia imejipanga kuwapoteza Yanga huku kocha wa timu hiyo Abdallah Kibadeni akisema, "Wachezaji wangu wamechoka kutokana na kuwa na mechi nyingi ndani ya muda mfupi, sasa nguvu nyingi nimezielekeza kwa Yanga hivyo ninatarajia matokeo mazuri kama zilivyopata timu zingine zilizocheza dhidi ya Yanga hivi karibuni."

HARAKATI ZA SIMBA
Simba walio katika kiwango cha juu, wataikabili Kagera Sugar ugenini kwenye Uwanja wa Kambarage leo.
Simba imeanza kampeni ya kuwania kushika usukani wa ligi ikiwa na pointi zake 39, baada ya kucheza mechi 17 huku wakiwa nyuma kwa pointi moja dhidi ya watani wao Yanga ambao wanaongoza kwa pointi 40.
Kwenye mzunguko wa pili wa ligi Kagera wameshinda michezo miwili kabla ya mchezo wa leo baada ya kuifunga kwa magoli 2-0 klabu ya Mbeya City kabla ya kuibwaga Majimaji 2-1 .
Kocha wa Simba, Jackson Mayanja, alisema, “Sibweteki na matokeo mazuri ninayopata hivi karibuni. Nitahakikisha ninaendeleza vipigo kwenye ligi ili kuiweka Simba kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa. Ninaamini wachezaji wangu wananielewa kwa kile ninachowalekeza. Nitawaongoza na kuendelea kuwapa mbinu za kutosha.”
Kocha wa Kagera, Adolf Richard, alisema, “Tumeyafanyia marekebisho makossa tuliyokuwa tukiyafanya, naamini sasa vijana wangu watafanya kile ambacho ni bora na kwa uwezo wao wa sasa naamini wataweza kuifunga Simba.

MECHI NYINGINE
Katika mechi nyingine za leo, Azam watakuwa wenyeji wa Mwadui FC kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam wakati Mbeya City itavaana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya. Ndanda wataikaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara. Toto Africans hao wataikaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na Majimaji watakuwa wenyeji wa Mgambo JKT Uwanja wa Majimaji, Songea.

Habari Kubwa