Jamhuri FC yapania kufuta sita za Yanga

07Jan 2020
Isaac Kijoti
Zanzibar
Nipashe
Jamhuri FC yapania kufuta sita za Yanga

KOCHA Mkuu wa Jamhuri, Mustafa Hassan maarufu 'Mu', amesema licha ya ubora wa Yanga huku ikiwa na wachezaji wengi wazoefu, mpira ni dakika 90 na lolote linaweza kutokea watakapokutana leo.

Timu hizo leo zitashuka katika Uwanja wa Amaan visiwani hapa katika kinyang'anyiro cha Kombe la Mapinduzi kilichoanza kutimua vumbi jana kwa Azam FC kuvaana na Mlandege huku Mtibwa Sugar ikimenyana na Chipukizi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mu alisema hawatarajii kufanya makosa kama ilivyokuwa mwaka jana na wamejiandaa kushinda mechi hiyo.

Alisema wamekuja kushindana na anamheshimu Boniface Mkwasa, Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, lakini hilo haliwezi kuwa kikwazo cha ushindi kwao.

"Yanga ni timu kubwa lakini mpira ni dakika 90 na tumejiandaa kushindana na kufanya vizuri mwaka huu," alisema.

Naye nahodha wa Jamhuri, Mohamed Juma Mohamed, alisema lolote linaweza kutokea na wamejiandaa vizuri kupambana na kutofanya makosa kwa kuruhusu mabao sita kama mwaka jana.

"Tupo vizuri na hatutarajii kukutana tena na bao sita kama mwaka jana tulivyocheza dhidi ya Yanga," alisema.

Kwa upande wake nahodha wa Yanga, Said Makapu, alisema wanaiheshimu Jamhuri kwa kuwa ni timu nzuri lakini lengo lao ni kushinda na kufika hatua ya fainali.

Azam FC ndio mabingwa watetezi wa mashindano hayo ambayo mwaka huu yanashirikisha timu nane za hapa nchini na yanachezwa kwa mtindo wa mtoano.

Habari Kubwa