Jeshi la Yanga limekamilika

18Jul 2019
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Jeshi la Yanga limekamilika
  • ***Ushindani wa namba wazidi kuongezeka huku wakimsubiri Zahera...

JESHI limekamilika! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya wachezaji wote wa Yanga kuwasili kambini mkoani Morogoro kwa ajili ya kushiriki maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh.

Hatua hiyo inakuja baada ya wachezaji wa kimataifa waliosajiliwa na Yanga kupata vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini.

Kikosi hicho ambacho kinanolewa na Kocha Msaidizi, Noel Mwandila, sasa kinamsubiri Kocha Mkuu Mkongomani Mwinyi Zahera, ambaye bado hajarejea kutoka likizo baada ya Timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kutolewa kwenye mechi za fainali za Kombe la Afrika.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kuwa kikosi cha Yanga sasa kipo kamili na kila mchezaji anashiriki vema programu za mazoezi zilizoandaliwa na benchi la ufundi la timu hiyo.

Saleh alisema kuwa wanafurahi kuona kila mchezaji anaonyesha bidii kwenye mazoezi, na hii inadhihirisha kwamba hakuna nyota atakayekuwa na namba ya kudumu kwenye kikosi hicho.

"Taarifa ambazo tunazo hapa kambini ni kuwa kocha mkuu atawasili nchini wakati wowote wikiendi hii, kwa sasa wachezaji wote tuliowasajili wamefika na wanaendelea na programu za mazoezi ambazo zinasimamiwa na Kocha Mwandila, ambaye anafuata maelekezo ya Zahera," alisema.

Mratibu huyo alisema kuwa ari ya mazoezi katika kikosi hicho ni kubwa na wachezaji wanadai kwamba muda wa kuanza ligi unachelewa.

"Kila kinachofanyika kocha Zahera anafahamu kwa sababu ni programu ya maandalizi ya msimu mpya, alishiriki kuiandaa, mambo mengine atakuja kuyaongeza yeye (Zahera) kama mkuu wa benchi la ufundi atakapofika," alisema Saleh.

Kiongozi huyo alisema kuwa wachezaji wote wa kigeni waliosajiliwa wapo tayari kuanza kutokana na kukamilisha taratibu za kupata vibali.

Aliwataja wachezaji hao wa kimataifa waliosajiliwa ni pamoja na Patrick Sibomana, Juma Balinya, Maybin Kalengo, Farouk Shikalo, Issa Bigirimana, Lamine Moro, Sadney Urikhob na Mustapha Selemani.

Kabla ya kuwakaribisha AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika mechi ya kirafiki kwenye tamasha la Siku ya Mwananchi litakalofanyika Agosti 4 mwaka huu, mabingwa hao wa kihistoria wataivaa Dodoma FC kwenye mchezo mwingine wa kirafiki utakaochezwa Julai 27 mwaka huu.