Jeuri yaendelea kutawala Yanga

24Jun 2022
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Jeuri yaendelea kutawala Yanga

WAKATI Kocha Mkuu wa Yanga, Nesredine Nabi, akimkingia kifua winga wake, Chiko Ushindi kupewa mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia timu hiyo katika msimu ujao, amesema wachezaji wake wanazidi kuimarika kuelekea mchezo wa fainali ya michuano ya Kombe la FA utakaochezwa Julai 2, mwaka huu Arusha.

Chiko aliyesaini mkataba wa miezi sita na mwisho wa msimu huu unafikia tamati kuhusiana na hatima yake, amekuwa kwenye sintofahamu kwa sababu hajafanya vyema kwa kipindi hicho cha mkataba wake.

Hata hivyo nyota huyo juzi alionyesha kiwango kizuri katika mchezo dhidi ya Polisi Tanzania, ambapo alifunga bao la pili dakika ya 17 huku lile na awali likipachikwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam kwa mabingwa wapya kuibuka na ushindi wa magoli 2-0.

Baada ya Chiko kufunga bao la pili, Nabi alinyanyuka na kushangilia kwa furaha na kugeukia jukwaa walilokaa viongozi wa Yanga na kuonyesha ishara ya ujumbe kwa viongozi hao kumwandalia mkataba mpya winga huyo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Nabi alisema anataka kumpa nafasi zaidi ya kucheza katika michezo miwili iliyosalia ya Ligi Kuu pamoja na mmoja wa fainali ya Kombe la FA ambapo watakutana na Coastal Union ya jijini Tanga.

Nabi alisema ana matarajio makubwa na Ushindi kwa sababu anajua uwezo wake na ana imani viongozi wa klabu hiyo watafuata mapendekezo yake ya usajili na wachezaji ambao wanatakiwa kubaki.

“Sijaanza kumjua Ushindi hapa Yanga, namjua muda mrefu lakini kuna maisha aliyapitia TP Mazembe ambayo yanatupa shida kuona kile alichonacho, unapomwona mazoezini ni tofauti na kwenye mechi,” alisema Nabi.

Aliongeza winga huyo anajua vyema kusakata kandanda ila kutokana na mazingira ya Ligi Kuu Tanzania ilimfanya kushindwa kuonyesha kiwango kizuri na sasa anapambana kuhakikisha katika michezo iliyosalia anamalizia.

Pia alimtaja Ibrahim Baka anatakiwa kuongezewa vitu kidogo ili kumjenga vyema kwa sababu itasaidia kupunguza gharama za kufanya usajili wa beki mpya kutoka nje ya nchi ambaye anaweza pia akashindwa kuonyesha kiwango kizuri.

Kuhusiana na mechi dhidi ya Polisi Tanzania, kocha huyo alisema haikuwa rahisi sana na hasa kipindi cha pili wapinzani wao waliingia kivingine na kusababisha kushindwa kutengeneza nafasi ya kupata mabao mengine.

"Niwapongeze wachezaji wangu wamepambana na kutumia nafasi vizuri kipindi cha kwanza na kufanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0, kipindi cha pili tulijaribu kufika lakini wapinzani walikuwa makini," alisema Nabi.

Aliongeza alifanya mabadiliko makubwa ya kikosi kwa kuwapa nafasi baadhi ya wachezaji ambao hawajacheza muda mrefu kama ilivyo kwa Baka kucheza na wengine kuwapumzisha.

"Kuumia kwa Zawadi Mauya kumesababisha baadhi ya wachezaji wasipumzike ikiwamo Khalid Aucho na Salum Abubakar (Sure Boy) kutopumzika katika mchezo wa leo (juzi)," alisema Nabi.

Wakati huo huo, kikosi hicho cha mabingwa kiliwasili salama jijini Mbeya kwa ajili ya mchezo dhidi ya Mbeya City utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Sokoine.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema wameamua kuondoka mapema ili kupata muda mzuri wa maandalizi ya kulipokea kombe lao.

"Michezo iliyobaki ni mechi za mazoezi ya kujiandaa na fainali ya Kombe la FA tutakaocheza Arusha, mikakati yetu ni kuchukua makombe yote msimu huu," Bumbuli.