JKT Mbweni, Mafunzo kibaruani

25Nov 2018
Renatha Msungu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
JKT Mbweni, Mafunzo kibaruani

WAKATI timu za netiboli za Uhamiaji na Jeshi Stars zimejitoa kushiriki katika mashindano ya Ligi ya Muungano, JKT Mbweni itawakaribisha Mafunzo kutoka Zanzibar katika mechi ya ufunguzi itakayochezwa kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa uliopo jijini Dar es Salaam, imeelezwa

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Ntiboli Tanzania (Chaneta), Judith Ilunda, alisema kuwa mechi hiyo ya ufunguzi utachezwa jioni na wanawakaribisha wadau wa mchezo huo kujitokeza kushuhudia mashindano hayo.

Ilunda alisema kuwa timu nyingine zilizothibitisha kushiriki mashindano hayo zimeshawasili jijini na ratiba kamili ya michuano hiyo itatolewa leo asubuhi.

"Mashindano yetu yanatarajia kuanza kesho (leo) hadi Desemba Mosi mwaka huu, mechi zote zitachezwa kwenye Uwanja wa Ndani," alisema kiongozi huyo.

Aliongeza kuwa uamuzi wa Uhamiaji na Jeshi Stars kujitoa katika mashindano hayo unatokana na wachezaji wa timu hizo kukabiliwa na majukumu mengine ya kikazi katika ofisi zao.

"Tumepokea barua kutoka kwa viongozi wa timu hizo, sababu walizotoa ziko nje ya uwezo wao, tunaziheshimu," Ilunda alisema.

Alizitaja timu nyingine za wanawake kutoka Tanzania Bara zitakazoshiriki kuwa ni pamoja na JKT Mbweni, Mgulani JKT, Magereza Moro, Polisi Moro na Polisi Arusha wakati wanaume watawakilishwa na Prisons, Smart, Talent, Chuo Kikuu na Muungano Dodoma.

Habari Kubwa