JKT Tanzania yaipa jeuri Mbeya City Bara

29Jun 2020
Somoe Ng'itu
Mbeya
Nipashe
JKT Tanzania yaipa jeuri Mbeya City Bara

USHINDI wa mabao 2-0 walioupata Mbeya City katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya JKT Tanzania iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa juzi, umeipa nguvu mpya timu hiyo iliyopo katika janga la kushuka daraja, imeelezwa.

Mbeya City sasa imefikisha pointi 33 ikiwa imeshuka dimbani mara 32, na hivyo kubakisha mechi sita ili kumaliza msimu wa 2019/20 unaotarajiwa kumalizika Julai 26, mwaka huu.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Mbeya City, Amri Saidi, alisema anawapongeza vijana wake kwa kufuata vema kikamilifu maelekezo yake ambayo yalizaa matunda katika mchezo huo.

Saidi alisema bado hawajakata tamaa ya kushuka daraja na wamejipanga kuendelea kupambana hadi dakika ya mwisho katika Ligi hiyo ya juu hapa Tanzania Bara.

Kocha huyo alisema ushindani wa ligi hiyo msimu huu ulikuwa tangu mwanzo na hivyo anaendelea kuwakumbusha wachezaji wake kuongeza umakini.

"Nimefurahi sana kwa ushindi wa jana (juzi), bado yuko kwenye mapambano, hatujakata tamaa, ushindi tuliopata umetusaidia kupata nguvu mpya kwenye vita tunayopigana, tunaamini tutafanikiwa," Saidi alisema.

Naye Kocha wa JKT Tanzania, Abdallah Mohammed "Bares", alisema kikosi chake kilikuwa na wakati mgumu kutoka kwa wapinzani wao ambao walitumia vema makosa waliyofanya wachezaji wake.

"Hatukuwa na siku nzuri, siwezi kuwalaumu wachezaji wangu, wamenipa matokeo mazuri katika mechi kadhaa zilizopita, bado tunaendelea kupambana ili tumalize vema msimu huu," Bares alisema.

Mabao ya Mbeya City katika mchezo huo wa raundi ya 31, yalifungwa na Patson Shigala na Peter Mapunda.

Habari Kubwa