JKT wainyima usingizi Yanga

09Feb 2019
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
JKT wainyima usingizi Yanga

BAADA ya kuambulia pointi mbili kati ya tisa katika michezo mitatu waliyocheza, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema kuwa wamejiandaa kusaka ushindi katika mechi ya kesho ili kurejesha morali katika kikosi chao.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, picha na mtandao

Yanga itashuka ugenini kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga kuwavaa wenyeji JKT Tanzania huku wakiwa na kumbukumbu ya kuambualia sare ya bao 1-1 katika uwanja huo dhidi ya Coastal Union, wiki moja iliyopita.

Akizungumza na gazeti hili Zahera, alisema kuwa wamejiimarisha zaidi na hataki kuona anapata matokeo kama aliyoyapata kwenye michezo iliyopita.

" Tumeangusha pointi kwenye michezo iliyopita, ndio hali ya mchezo, lakini ili kuendelea kuwa na morali na kasi yetu ni lazima tupate ushindi katika mchezo wa Jumapili (kesho)," alisema Zahera.

Kocha huyo alisema kuwa hakuna ambaye anapaswa kulaumiwa kutokana na matokeo ya mechi tatu zilizopita, kwa sababu wachezaji wake walijitahidi kupambana lakini hali ngumu ya mchezo ndio ilisababisha kushindwa kupata ushindi.

"Kikubwa ni kujipanga na kuhakikisha tunatengeneza nafasi nyingi na kuzitumia, sitarajii mchezo mwepesi hasa ukizingatia tunacheza ugenini na wapinzani wetu nao watakuwa wamejipanga kupata matokeo mazuri," alisema Zahera.

JKT Tanzania itaikaribisha Yanga ikiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Biashara United.

Matokeo ya juzi dhidi ya Singida United imeifanya Yanga kufikisha pointi 55 na kuendelea kuongoza katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 20.

Habari Kubwa