Julio aanza majigambo akikaribia Ligi Kuu Bara

02Nov 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Julio aanza majigambo akikaribia Ligi Kuu Bara

KOCHA Mkuu wa timu ya Dodoma FC ya Dodoma, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’, amesema matokeo mazuri ambayo timu yake inapata katika mechi za Ligi Daraja la Kwanza yanatokana na wao kujipanga na si kubebwa kama baadhi ya wadau wanavyosema.

KOCHA Mkuu wa timu ya Dodoma FC ya Dodoma, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’,.

Akizungumza na gazeti hili jana, Julio, alisema kuwa anaamini kikosi chake kina nafasi ya kupanda daraja na kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao kwa sababu wamejipanga kuendelea kupambana ili watimize malengo waliyoyaweka.

Beki na kocha huyo wa zamani wa Simba alisema pia ligi hiyo ni ngumu na ina changamoto mbalimbali huku akiweza wazi kukukutana na ushindani kwenye michezo yote wanayocheza.

“Hakuna mechi rahisi, tunapambana katika kila mechi, hatubebwi, hata ukiangalia matokeo yetu, mechi nyingi tulizoshinda tumecheza ugenini, tutaendelea kupambana tutakaporudi kumalizika michezo ya nyumbani," alisema Julio.

Baada ya juzi kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Toto Africans, Dodoma FC imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa na pointi 18, ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine katika kundi lao ikiwamo Alliance ambayo imekuwa mshindani.

Timu sita kutoka katika Ligi Daraja la Kwanza zitapanda daraja na kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao wa 2017/18.