Juma Abdul: Anaturudisha enzi za kina Mavumbi

09Mar 2016
Adam Fungamwango
Dar
Lete Raha
Juma Abdul: Anaturudisha enzi za kina Mavumbi

ALIACHIA kiki kali iliyokwenda moja kwa moja hadi wavuni na kuisawazishia Yanga bao ambalo yeye mwenyewe ndiye aliyekuwa amejifunga baada ya kugongwa na mpira uliopigwa na Kipre Tchetche.

Abdul Juma wa Yanga akipiga mpira huku beki wa Prisons akijaribu kumzuia.

Kiki hiyo aliipiga mita zilizopungua 25 baada ya shambulizi kali na mpira ukaokolewa kizembe na mabeki wa Azam, kabla ya kukutana na beki huyo, akautendea haki.

Dakika kadhaa kabla ya goli hilo alifanya jaribio kama hilo, alipoukuta mpira unazagazagaa kwenye nje ya 18 na kuachia fataki kali lililopanguliwa na kipa Aishi Manula na kuokolewa na mabeki wake.

Beki huyu si mwingine ila ni Juma Abdul anayecheza beki wa kulia aliyezaliwa Novemba 10 mwaka 1992.

Kwa miaka ya karibuni na aghalabu sana kuona hata mastraika wakipiga mashuti makali kiasi kile na badala yake wamekuwa wakifunga magoli laini tu.

Zamani magoli ya aina ile yalikuwa yakifungwa si na mastraika pekee yao au viungo kama kina Athumani China na Hamisi Gaga, lakini hata mabeki hasa wa pembeni walikuwa na uwezo huo wa kuachia mafataki ya 'kufa mtu' wakiwa mbali na lango.

Mabeki kama kina Kenneth Mkapa, Rafael Paul, Kihwelo Mussa, Mavumbi Omari na wengine, walikuwa na uwezo na kwenda mbele kusaidia mashambulizi, huku wakiwa wamejaliwa kuwa na mashuti makali na yenye uwezo wa kulenga lango, hivyo kuzisaidia timu zao kufunga magoli wakati mastraika wakiwa wamebanwa.

Mwaka 1990, Simba iliifunga Yanga bao 1-0 lililofungwa na beki wa kushoto Mavumbi Omari alipoachia kombora kali dakika ya sita tu ya mchezo akiwa kiasi cha mita 35 hivi, shuti lililokwenda moja kwa moja hadi wavuni na kumuacha kipa Sahau Kambi akiutazama kwa macho.

Mashuti ya aina hiyo kwa miaka ya karibuni yamekuwa haba sana kuyashuhudia kwenye viwanja vya soka, lakini kwa mbali beki huyo ameanza kuwakumbusha mashabiki wa soka hasa wale wa zamani kuwa mambo yale yanarudi tena.

Alisajiliwa na Yanga akitokea Mtibwa Sugar mwaka 2012, lakini hakuwa mchezaji wa kutegemewa, ila kadri muda ulivyozidi kusonga mbele ndipo amejipambanua kuwa mmoja wa mabeki bora kwa sasa nchini.

Mchezaji huyo amewahi pia kuichezea Toto African ya Mwanza kwenye Ligi Kuu, soka lake akianzia Kingalu Kids mkoani Morogoro.

Baada ya kumaliza mkataba wa miaka miwili akiwa Yanga, aliongezwa mingine miwili ambayo inamalizika msimu huu na sasa siku tatu zilizopita wamemuongezea mkataba mwingine wa miaka miwili utakaoisha 2018.

Sidhani kama viongozi wa Yanga wanapepesa macho juu ya kumuongezea mkataba mwingine mchezaji huyo anayeonyesha uwezo mkubwa kwa sasa.

Yoyote atakayesema kuwa alibahatisha atakuwa amekosea.
Oktoba 21 mwaka jana, kwenye ligi ya msimu huu alifunga goli linalofanana na aliliofunga dhidi ya Azam FC.

Goli hilo alilifunga akicheza dhidi ya Toto African, ikiwa ni dakika ya tisa tu baada ya pambano kuanza Uwanja wa Taifa, alipotandika kombora kali akiwa kiasi cha mita 20 na mpira kujaa wavuni, akiisaidia Yanga kushinda mabao 4-1.

Habari Kubwa