JWTZ kushiriki michezo ya majeshi Dunia

04Jul 2019
Faustine Feliciane
Nipashe
JWTZ kushiriki michezo ya majeshi Dunia

JESHI la Wananchi la Tanzania (JWTZ), litatuma wanamichezo kushiriki michezo mitatu tofauti katika michuano ya Dunia ya Majeshi itakayofanyika nchini China kuanzia Oktoba 18 hadi 27, mwaka huu.

Kanali Joseph Bakari.

Katika michezo hiyo itakayoshirikisha wanamichezo 10,000 kutoka nchi wanachama wa Baraza la Dunia la Michezo ya Majeshi (CISM), Tanzania itashiriki michezo ya riadha, ngumi na mieleka.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwakilishi wa Tanzania CISM lililo na makao makuu nchini Ubelgiji, Kanali Joseph Bakari, alisema Baraza hilo litasaidia baadhi ya gharama ya timu hiyo ya JWTZ.

Alisema kwa upande wa baraza hilo, kwa sasa wapo kwenye kipindi cha maandalizi mpaka mwishoni kwa mwezi huu.

"Kwa kuwa mimi ni mwakilishi wa nchi yetu kwenye baraza hili na kitengo changu kinahusika na michezo hii, nafahamu Tanzania itashiriki kwenye michezo hiyo mitatu," alisema Kanali Bakari.

"Kuna michezo mingi sana inayoshirikishwa mingine kutokana na mazingira ya Afrika wachezaji kutoka Afrika hawawezi kushiriki, michezo kama ya kuteleza kwenye barafu na mingineyo, kwa Tanzania mwaka huu watashiriki kwenye michezo hiyo mitatu," alisema.

Habari Kubwa