Kadi ya Yondani kimbembe mechi Simba vs Yanga

10Feb 2016
Faustine Feliciane
Nipashe
Kadi ya Yondani kimbembe mechi Simba vs Yanga

UONGOZI wa Yanga umesema upo 'njia panda' juu ya adhabu kukosa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara inayomkabili beki wake wa kati na naodha msaidizi wa klabu hiyo, Kelvin Yoindani, kutokana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwa kimya.

Yondani, beki wa zamani wa Simba, alilimwa kadi nyekundu na refa Andrew Shamba baada ya kupigana na daktari wa Coastal katika dakika ya 90+9 ya mechi ya raundi ya 16 ambayo Wanajangwani walilala 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga Januari 30.

Wakati Kanuni za Ligi za TFF zinataja adhabu ya mechi tatu na faini ya fedha kwa mchezaji anayepiga au kupigana uwanjani, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa wameomba ufafanuzi kutoka TFF kuhusu adhabu hiyo ambayo itamlazimu beki huyo kukosa mechi ijayo ya watani baada ya mechi yao dhidi ya Mtibwa Sugar kupigwa kalenda.

"Ni jambo ambalo tunasubiri wenzetu wa TFF watupe ufafanuzi, lakini mpaka jana (juzi) walituambia bado kamati husika ilikuwa haijakaa.., tunasubiri," alisema Muro.

Ibara ya 37(3) cha Kanuni za Ligi za TFF toleo la 2015, kinasema: "Mchezaji atakayetolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kupiga/Kupigana, atasimama kushiriki michezo mitatu (3) inayofuata ya klabu yake na atalipa faini ya shilingi laki tano (Tsh.500,000)."

Tayari Yondani ameshakosa michezo miwili wakati timu yake ilipocheza dhidi ya Tanzania Prisons na dhidi ya JKT Ruvu.

Habari Kubwa