Kagera Sugar, Mwadui ni kufa na kupona leo

08Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR
Nipashe
Kagera Sugar, Mwadui ni kufa na kupona leo

HATIMA ya timu zinazowania nafasi ya kubakia au kupanda daraja kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kufahamika baada ya kumalizika kwa mechi za marudiano za Play Off zitakazochezwa leo kwenye viwanja viwili tofauti nchini.

Kagera Sugar.

Mechi ya kwanza itakuwa kati ya Kagera Sugar dhidi ya Pamba FC ambayo itachezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba Mjini Bukoba na nyingine itawakutanisha Mwadui FC dhidi ya Geita Gold FC kwenye Uwanja wa Mwadui Complex mkoani Shinyanga.

 

Katika mechi za kwanza zilizochezwa wiki iliyopita, matokeo yalikuwa ni sare ya bila kufungana na inamaanisha kuwa timu zitakazopata ushindi leo, zitakuwa zimekata tiketi ya kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao wa 2019/20.

Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime, aliliambia gazeti hili kwamba wamejiandaa kupambana katika mechi ya leo ili wapate ushindi na hatimaye kubakia kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu mwingine zaidi.

Maxime alisema mechi hiyo ya marudiano haitakuwa nyepesi, kwa sababu kila timu ina nafasi sawa na lolote linaweza kutokea katika mchezo wa soka.

"Inaitwa hakuna kulala, ukizembea unapigwa na unashuka daraja, kwa mapenzi ya Mungu, naamini tutafanya kila ambacho tunakitarajia," alisema kocha huyo.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Geita, Pius Kimisha, alisema kuwa wachezaji wote wa Geita Gold wako katika hali nzuri na wanachoomba ni kuona wanajituma na hatimaye kupata ushindi katika mchezo wa leo.

"Tunatarajia na tulijua mapema kuwa mechi za Play Off ni ngumu, ila nafasi ya kutimiza ndoto zetu kwa kupanda daraja bado zipo, tunaomba ushirikiano tulioupata kutoka kwa wadau wetu uendelee," alisema Kimisha.

Tayari Namungo FC na Polisi Tanzania zimeshapanda daraja wakati zilizoteremka hadi Ligi Daraja la Kwanza ni African Lyon ya Dar es Salaam na Stand United ya Shinyanga.

Habari Kubwa