Kagera yahitaji wachezaji nane

22Jul 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Kagera yahitaji wachezaji nane

BAADA ya kufanikiwa kuinusuru timu katika janga la kushuka daraja, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Francis Baraza, ameweka wazi anahitaji kusajili wachezaji nane wapya ili kuimarisha kikosi chake kuelekea katika msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kagera Sugar iliyojikusanyi pointi 40 ilimaliza msimu uliopita ikiwa katika nafasi ya 12, ambayo ni ya mwisho huku timu zilizofuatia, Mtibwa Sugar na Coastal Union zikiangukia kucheza mechi za mchujo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Baraza alisema anahitaji kuongeza nguvu katika kikosi chake na ili kuwa imara atasajili wachezaji wasiopungua nane kwa kuzingatia nafasi mbalimbali alizopendekeza.

Baraza alitaja nafasi hizo ambazo anataka kuziboresha ni pamoja na beki wa pembeni, beki wa kati, kiugo mkabaji, mshambuliaji mmoja wa pembeni na washambuliaji halisi wawili.

"Nahitaji kuimarisha hizo nafasi, kesho (leo) nitakutana na viongozi wangu kwa ajili ya kuwapa ripoti ya awali na mwisho wa wiki hii nitakabidhi ripoti kamili kuhusu mikakati yangu kuelekea msimu mpya," alisema Baraza.

Kocha huyo alisema kikao cha leo, hakitaonyesha usajili ila kitatoa mwongozo wa mahitaji muhimu ya timu hiyo ikiwamo programu za maandalizi ya msimu ujao na kuhakikisha hawarudii makosa yaliyojitokeza katika msimu uliomalizika.

Habari Kubwa