Kagera yapania tatu za Simba Kaitaba leo

21Apr 2021
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
Kagera yapania tatu za Simba Kaitaba leo

WAKATI leo wakiwakaribisha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Benchi la Ufundi la Kagera Sugar limesema limejipanga vizuri kukutana na Simba katika mchezo wao wa leo watakaoucheza mkoani Kagera, na kuahidi kutoa ushindi wa hali ya juu.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka mkoani Kagera, Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Francis Baraza, alisema licha ya kwamba wanakutana na timu kubwa, wamejipanga kuhakikisha wanapata pointi zote tatu wakiwa katika uwanja wa nyumbani wa Kaitaba.

“Tumejipanga vizuri kukutana na Simba katika mchezo wetu wa kesho( leo), nimejipanga kupata pointi tatu nikiwa na lengo la kuiweka mahali pazuri timu yangu, ninaomba mashabiki waendelee kutupa ushirikiano”alisema Baraza.

Kocha huyo alisema mchezo huo utakuwa mgumu na wenye ushindani mkubwa kutokana na kila timu ambayo inashiriki Ligi Kuu imejipanga vizuri kupata pointi tatu kwenye kila mchezo ambao inaucheza ili kuhofia kushuka daraja.

“Mchezo utakuwa na ushindani kwa sababu kila timu msimu huu imejipanga kupata matokeo, wachezaji wangu wanaendelea vizuri kila mmoja ana morali ya ushindi kuelekea katika mchezo huo,” alisema.

Alisema makosa madogo madogo ambayo aliyabaini kwenye mchezo uliopita ameyafanyia kazi na kudai  hayawezi kujitokeza kwa mara nyingine huku akiahidi mashabiki wake kuiweka juu timu hiyo ambayo alikabidhiwa baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Mecky Maxime kutupiwa virago.

Habari Kubwa