Kagere: Hatuna presha kuwavaa TP Mazembe

22Mar 2019
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Kagere: Hatuna presha kuwavaa TP Mazembe

SIKU moja baada ya Shirikisho la Soka Afrika ‘CAF’ kupanga droo ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere, amesema hana hofu na timu waliyopangiwa nayo.

Katika droo hiyo, Simba imepangwa kuumana na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo mchezo wa kwanza utachezwa hapa nchini kati ya Aprili 5 na 6 mwaka huu.

Kagere, akizungumza na gazeti hili, alisema kama timu hawana hofu na mpinzani wao kwa kuwa kila mchezo ni kujipanga kuweza kupata ushindi.

Alisema anafahamu TP Mazembe ni moja ya timu kubwa Afrika, lakini pia Simba si timu ndogo na ndio sababu imefika hatua ya robo fainali.

“Tunajipanga kwa mchezo huo… hatua hii hakuna timu nyepesi na wala hakuna timu yenye uhakika wa kusonga mbele kabla ya dakika 90,” alisema Kagere.

Alisema anafahamu kocha wao, Patrick Aussems ataandaa mbinu za kuwafikisha hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya vilabu Afrika.

“Ushindi tunaoupata kwenye michezo yetu unachangiwa pia na mashabiki wetu kwa hamasa kubwa wanayotupa…waendelee kutusapoti na kutupa hamasa kwenye hatua hii,” aliongeza kusema.

Simba imetinga hatua hiyo baada ya kushika nafasi ya pili kwenye kundi lao, wakati hatua ya makundi ikichomoza nyuma ya Al Ahly ambao wamepangiwa kucheza na Mamelodi ya Afrika Kusini.

Habari Kubwa