Kagere, Miquissone warejea nchini

23Nov 2020
Saada Akida
Arusha
Nipashe Jumapili
Kagere, Miquissone warejea nchini

​​​​​​​NYOTA wawili wa kimataifa wa Simba mshambuliaji, Meddie Kagere na winga, Luis Miquissone, wamerejea nchini wakitokea kuzitumikia timu zao za Taifa za Rwanda na Msumbiji, tayari kuanza maandalizi ya kuwavaa Plateau United ya Nigeria katika mechi ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kagere na Miquissone walikosa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi Coastal Union uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini, Arusha baada ya kuchelewa kurejea nchini.

Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck alisema anatarajia wachezaji hao watakuwapo katika msafara wa kuelekea Nigeria na tayari kwa mchezo wao huo wa kwanza wa kimataifa.

"Walichelewa kujiunga na timu kwa kuwa walikuwa na majukumu kwenye timu zao za Taifa, wataungana na kikosi mapema na watakuwa miongoni mwa wachezaji watakaokuwa katika majukumu ya klabu kwenye michuano ya kimataifa," alisema Sven.

Kagere ambaye alikuwa majeruhi ameliambia gazeti hili sasa yupo fiti kwa ajili ya kurejea uwanjani na katika kuhakikisha timu yake inafanya vizuri katika mechi zote zinazowakabili.

"Baada ya kukaa nje muda mrefu na kupata matibabu, sasa niko fiti na nipo tayari kurudi uwanjani kusaidia timu yangu kufanya vizuri katika michezo iliyopo mbele yetu,” alisema Kagere.

Kagere ametua nchini juzi akitokea Rwanda, wakati Miquissone ameungana na kikosi hicho jana.

Simba itavaana na Plateau United katika  mchezo wa kwanza utakaochezwa kati ya Novemba 27 na 29, mwaka huu huku ikiwakaribisha wageni hao Desemba 6 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini.

Habari Kubwa